Walimu msiwawekee vikwazo watoto wanaoanza shule : DC Shinyanga.

 
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ofisini kwake leo.


Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
 
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amewataka wazazi kuhakikisha Watoto wote wanaotakiwa kwenda shule kwa Mwaka wa Masomo 2023,wanaripoti shuleni kwa wakati.
 
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo amewaomba wakuu wa shule pamoja na walimu wengine kutoweka vikwazo vyovyote kwa watoto wanaotakiwa kwenda shuleni  huku akiwasisitiza wanawapokea bila kujali changamoto zao.
 
DC Mboneko amewasisitiza wazazi na walezi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa watoto ikiwemo kuwanunulia sale za shule, vifaa na mahitaji mengine ili wasome kwa bidii na kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii na Taifa kwa ujumla.
 
“Nitoe wito kwa viongozi wote kwenye ngazi zetu za vitongozi, vijiji, mitaa, kata na Wilaya kwa ujumla kuhakikisha kwamba watoto wote wanaotakiwa kuwa shuleni wawepo shuleni lakini pia kwa watoto ambao wameandikishwa kuanzia darasa la awali na darasa la kwanza”.
 
“ Nitoe wito kwa wakuu wa shule pamoja na walimu wengine kwamba tusiweke urasimu wowote kwa watoto ambao wanatakiwa wawe shuleni na jambo hili katika baadhi ya maeneo tayari limeshasikika kuna urasmi ambao unawekwa na walimu kwamba watoto hawa wasipokelewa kwa sababu hawana sale, hawana viatu, hawana vifaa vya shule mimi niwahimize wazazi na walezi tujitahidi kuwanunulia mahitaji ya shule watoto wetu ili waende shuleni lakini pia na wale wa awali na darasa la kwanza wanaweza kuanza na nguo za nyumbani”.amesema DC Mboneko
 
Mboneko amesema tangu shule zifunguliwe hakuna changamoto iliyojitokeza ambapo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan huku akieleza kuwa shule zote za Wilaya ya Shinyanga zinaendelea vizuri na zoezi la kupokea wanafunzi.
 
Dc  Mboneko amekumbusha  viongozi  kuanzia ngazi ya Mtaa, wanafunzi, wazazi na walezi pamoja na jamii kwa ujumla kutofumbia macho  taarifa za ukatili, na kwamba wanapaswa kutoa taarifa kwa wakati sehemu husika ili hatua zaidi zichukuliwe.
 
“Suala la kumlinda mototo na ukatili nila wote siyo serikali tu jamii pia inapaswa kushirikiana na serikali lakini niwaombe wazazi wawe na utamaduni wa kukaa na kuzungumza na watoto wao hii desturi itasaidia wazazi kujua hali ya mototo wake kila siku”. amesema DC Mboneko
 
“Watoto, wazazi na walezi pamoja na jamii linapotokea suala hili la ukatili wa kijinsia basi litolewe taarifa haraka sana ili hatua za kisheria zichukuliwe, utakuta mtu amefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ameshaoga ametoa kila kitu na huwezi tena kupata ushahidi kwahiyo niombe sana linapotokea jambo hili litolewa taarifa haraka mtu asifiche taarifa hata kama ni kiongozi wa eneo husika ameshiriki kwa namna moja ama nyingine tutamchukulia hatua”.
 
“Wazazi na walezi pia waendelee kufuatilia masuala yote ya elimu kwa watoto wao kwamba wanakwenda shuleni na wanarudi nyumbani salama lakini pia wazazi waache tabia ya kuozesha watoto niwatake wasubiri mpaka ufike ule umri wao wa kwenda kuolewa ndiyo waolewe kwa sababu ukatili mwingine unafanyika ndani ya familia na nje ya familia lazima tuwajengee watoto uwezo wa kutoa taarifa kwahiyo ni vizuri sana wazazi wakawa na utamaduni wa kuongea na watoto wao”. amesema DC Mboneko

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post