TCA yawatoa hofu wakulima, yaahidi kununua Pamba yote iliyozalishwa.


Zao la Pamba likiwa kiwandani kwa ajili ya kuchambuliwa ili kupata Pamba nyuzi na Pamba Mbegu.

 

Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba nchini (TCA), Boaz Ogolla.

 

Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.

 

CHAMA cha Wanunuzi wa Pamba nchini (Tanzania Cotton Association) kimesema kitahakikisha kinanunua pamba yote ya wakulima iliyozalishwa kwa bei elekezi iliyopangwa na serikali pia watazingatia bei ya soko la Dunia.

 

Hatua hiyo inakuja baada ya wakulima kulalamika kununuliwa pamba yao kwa bei ya shilingi 1060 tofauti na msimu wa mwaka jana (2022/23) ambapo walinunuliwa kwa shilingi 2000 kwa kilo moja.

 

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Katibu wa TCA, Boaz Ogolla amesema wanaipongeza serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji katika sekta ya pamba na kuwahakikisha wakulima kuwa watanunua pamba yote iliyozalishwa nchini kwa bei elekezi iliyotolewa na serikali.

 

Ogolla amesema bei ya shilingi 1060 kwa kilo moja waliyoanza nayo mwaka huu, ni bei halisi ya soko la kimataifa na kwa miaka mitano iliyopita kulikuwa na hisia kuwa hakuna pamba ya kutosha kwenye soko la kimataifa.

 

‘’leo bei hii ya 1060 kwa kilo, ndiyo bei halisi ya soko la kimataifa…tulijitahidi sana kupata bei ya 1060 iliyotangazwa, huwa tunapenda kutoa motisha kwa mkulima, bei ikipanda huwa tunashindana sana na mkulima atapata bei nzuri’’ amesema Ogolla.

 

Amefafanua kuwa kinachosababisha bei ya pamba kutegemea soko la dunia, ni kwa sababu viwanda vya ndani haviwezi kukidhi mahitaji na badala yake wanategemea inunuliwe na viwanda nje ya Tanzania.

 

Amewataka wakulima kuongeza tija ya uzalishaji wa pamba ili kupata mazao ya kutosha kwani hata bei ikishuka kwenye soko la dunia wakulima watapata fedha nyingi na pia wakulima wapate huduma za ugani na pembejeo hata soko likishuka wabaki sehemu salama.

 

Ameongeza kuwa ununuzi wa Pamba katika msimu huu wa 2023/24 utafanyika kwa mifumo miwili ambayo ni Simiyu Model na Mfumo wa Amcos, mifumo ambayo inaruhusu wanunuzi wa pamba katika mkoa wa Simiyu kununua bila kutumia vyama vya ushirika.

 

‘’Mwongozo unatuelekeza kuwa na mifumo miwili kama tuliyotumia mwaka jana, Mfumo wa kununua kwa kutumia Amcos na Simiyu Model…Simiyu model imechukua wilaya zote za Simiyu, Magu na Kwimba ambapo mnunuzi anaweka kituo chake na haikuzuii kutumia amcos’’ amesema Ogolla.

 

Kwa upande wao wakulima wa Pamba wilaya ya Bariadi wamesema serikali imetangaza bei elekezi ambayo haikidhi gharama za uzalishaji wa pamba kutoka kuandaa shamba hadi kuvuna.

 

Masunga Jisena, Mkazi wa Nyanguge ameiomba serikali kuongeza bei ya pamba ili wakulima waweze kunufaika kwa gharama za uandaaji wa shamba la pamba ni kubwa.

 

‘’Pamba ina bidhaa nyingi sana katika mnyororo wa thamani, lakini wakulima hatuthamini, tunapewa bei ndogo sababu hatuwezi kukataa kulima pamba…mwaka jana bei ilipanda lakini mwaka huu bei imeshuka na hatujui sababu’’ alisema Jisena.

 

Naye Ng’huma Jocha amewataka wanunuzi wa Pamba kuongeza bei ya kununulia zao hilo ili kuwatia moyo wakulima hao vinginevyo wataacha kulima pamba na kuanza kuzalisha mazao mengine kama alizeti, mahindi na mpunga.

 

MWISHO.

 

Magari yaliyobeba zao la Pamba yakishushwa kwenya maghala baada ya kukusanywa kutoka vijijini tayari kwa ajili ya kuchambuliwa.


Magari yaliyobeba zao la Pamba kutoka vijijini yakishusha Pamba kwenye kiwanda cha Kuchambua Pamba cha Alliance Ginnery kilichopo Kasoli wilayani Bariadi.



Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba nchini (TCA) Boaz Ogolla ambaye pia ni Meneja wa Kiwanda cha Kuchambua Pamba cha Alliance Ginnery kilichopo Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu.





 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post