Mkuu wa Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu Faidha Salim akizungumza na wakati wa Hafla ya kupokea madawati 50 yaliyotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya shule ya Msingi Laini 'B'. |
Na Derick Milton Simiyu.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Laini ‘B’ katika
Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu, sasa hawatakaa chini baada ya
kupatiwa Madawati ya kutatua changamoto hiyo kutoka Benki ya NMB.
Shule hiyo yenye watoto 1062, wasichana wakiwa 564
na wavulana 498 ilikuwa na uhitaji wa madawati 50, ambapo baadhi ya wanafunzi
walilazimika kukaa chini darasani wakati wa masomo.
Katika hafla ya kupokea madawati hayo iliyofanyika
jana kwenye shule hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule Kitto Albert amesema kuwa
wanafunzi wa madarasa ya chini baadhi yao wamekuwa wakikaa chini.
Amesema kuwa hali hiyo imesababishwa na wingi wa
wanafunzi shuleni hapo, huku akieleza kuwa kukaa chini kwa wananfunzi hao
kulisababisha wajifunze katika mazingira magumu.
Albert amesema kupatiwa msaada wa Madawati hayo
kutoka Benki ya NMB, imemaliza kabisa changamoto ya ukosefu wa Madawati shuleni
hapo, ambapo ameishukuru benki hiyo kwa msaada wake.
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi Seka
Urio amesema kuwa, kama wadau wa maenedeleo nchini wanao wajibu wa kushirikiana
na serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Amesema kuwa NMB kwa mwaka 2022, ilitenga zaidi ya
Bilioni 6 kutoka kwenye faida yake, kwa ajili ya kurudisha kwa wananchi ambapo
wamekuwa wakisaidia katika sekta za Elimu, Afya pamoja na Majanga.
“ Leo tunakabidhi Madawati 50 yenye thamani ya Sh.
Milioni 3.6, kwenye shule hii ya Laini ‘B’, huu ni ushiriki wetu kwenye
shughuli za maendeleo kama benki ambayo inaoongoza tanzania, na tunao wajibu wa
kurudisha kwa jamii, kwani kwa mwaka jana tu tulitenga zaidi ya Bilioni 6,”
alisema Urio.
Kabla ya kupokea madawati hayo Mkuu wa Wilaya hiyo
Faidha Salim ambaye alikuwa mgeni rasmi akizungumza, amewataka wanafunzi na
walimu kuhakikisha wanatunza madawati hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.
“ Tunawashukuru sana NMB kwa msaada wetu, sasa
kuanzia leo watoto wa shule hii hawatakaa chini, changamoto hiyo imekwisha,
tunawashukuru kwa kumaliza hili tatizo, wanafunzi na walimu sasa wamepata
mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunza,” amesema Salim.
Aidha kiongozi huyo ameiomba benki hiyo kuendelea
kusaidia changamoto ya madawati kwenye shule nyingine, kwani ndani ya Wilaya
yake yenye shule za msingi 98 kuna changamoto ya ukosefu wa madawati zaidi ya
3000.
Mosea Bahame na Habi Gibishi ni wanafunzi wa shule
hiyo, wameishukuru benki ya NMB kwa kuwatatulia changamoto ya kukaa chini,
ambapo wameeleza walikuwa wanapata shida ya kupata vikohozi kutokana na vumbi.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment