Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
JESHI la Polisi Mkoa wa Simiyu limewataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuhakikisha wanazisalimisha ndani ya muda uliotolewa na serikali na kabla ya msako mkali utakaofanyika hivi karibuni.
Akizungumza leo na waandishi wa Habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi Edith Swebe amewataka wanaomiliki silaha kuzisalimisha vituo vya polisi, ofisi za watendaji wa vijiji na kata.
‘’Ninatoa wito kwa wananchi wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, wazisalimishe silaha hizo kwenye vituo vya polisi na kwa watendaji wa kata..zitapokelewa katika kipindi hiki cha msamaha’’ amesema.
Ameongeza kuwa hadi sasa zimebaki siku 19 kwa ajili ya usalimishaji wa silaha na baada ya hapo msako mkali utaanza kwa watu wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.
Ameongeza kuwa msako huo utafanyika nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wanakamatwa, ikizingatiwa kuwa Mkoa wa Simiyu unapakana na hifadhi ya Serengeti ambapo ujangili hufanyika.
MWISHO.
Post a Comment