Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassani imeendelea kutekeleza ujenzi wa vyumba vya Madarasa ya shule za Msingi kupitia Mradi wa BOOST ambao umewaondolea wananchi adha ya uchangiaji.
Wamesema miradi hiyo ambayo imeanza kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, imeonyesha mafanikio na kwamba madarasa yanajengwa kwa viwango na mfano pia yatapunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.
Wakizungumza jana na waandishi wa Habari, Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wameipongeza serikali kwa kuanzisha utaratibu wa kujenga vyumba vya madarasa vilivyokamilika vikiwa na vyoo pamoja na madawati.
Samwel Loth, Mkazi wa Maswa aliipongeza serikali kwa kutekeleza miradi hiyo na kuwaondolea wananchi adha ya uchangiaji ambao ulikuwa unasababisha vyumba vya madarasa kutokukamilika kwa wakati.
Alisema ujenzi wa miradi ya BOOST inayotekelezwa na serikali, umetengewa fedha za kutosha ili kuhakikisha ujenzi wake unakamilika kwa wakati ili wanafunzi waweze kusoma katika madarasa ya kisasa.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Shishiyu, Samson Serengeta alisema mradi wa BOOST imeipunguzia msongamano shule mama (Shishiyu) yenye wanafunzi 1656.
Alisema kupitia mradi huo ambao wananchi hawachangishwi na unaosimamiwa na serikali moja kwa moja, umesaidia kuondoa msongamano wa wanafunzi madarasani.
‘’Shule ya msingi Shishiyu, darasa moja lina wanafunzi 200 mpaka 300, hivyo ni vigumu sana mwalimu kufundisha darasa lenye wanafunzi 300 na wakaelewa kwa pamoja…kupitia mradi wa BOOS tunajivunia wazo la Rais Samia’’ alisema.
Alifafanua kuwa, kupitia shule Mama ya Shishiyu walipokea shilingi mil. 348.5 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya iliyosajiliwa kwa jina la Majengo yenye mkondo mmoja na hadi sasa wameshatumia shilingi mil. 332.7.
Aliongeza kuwa, wananchi walishirikishwa juu ya utekelezaji wa mradi huo kupitia mikutano ya hadhara ambapo wananchi waliridhia kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.
Modestus Makubi, Mwenyekiti wa shule ya Msingi Shishiyu aliipongeza serikali ya Rais Dk. Samia kwa kusimamia na kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya elimu ya msingi.
Alisema kupitia mradi wa BOOST, shule ya msingi Shishiyu itapanuka kutokana na shule ya mwanzo kuelemewa na idadi ya wanafunzi hali iliyosababisha kudorora kwa ufundishaji na ujifunzaji.
Mtendaji wa Kata ya Shishiyu, Maduhu Samson alimpongeza Rais Dk. Samia kwa kuwaletea wananchi wa Shishiyu shilingi mil. 348 ili kuwapunguzia adha ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Alisema baada ya kutolewa fedha hiz, waliitisha mikutano ya vijiji ili kuwatangazia wananchi ili wafahamu fedha zilizoleta na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia.
‘’Baada ya kupokea fedha hizo, tuliwatangazia wananchi kuwa serikali imeleta mil. 348.5, tuliwataarifu wananchi kuwa hawatashiriki shughuli yoyote bali wanatakiwa kutoa eneo…tumejipanga kulinda mradi na kuhakikisha vifaa hivi havipotei’’ alisema.
MWISHO.
Fundi Ujenzi akiendelea na shughuli ya ujenzi wa ukuta kwenye darasa la awali la shule ya Msingi Majengo iliyopo kijiji cha Shishiyu wilayani Maswa Mkoani Simiyu, mradi unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi Mil. 348.5.
Modestus Makubi, Mwenyekiti wa shule ya Msingi
Shishiyu akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya usimamizi wa mradi wa BOOST unaotekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Post a Comment