Na Derick Milton, Bunda-Mara.
Kutokana na uwepo wa Changamoto ya Mabadiliko ya tabia nchi,
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imewasisitiza wakulima wa zao la
mpunga nchini kutumia teknologia ya kilimo shadidi kwenye zao hilo ili
kukabiliana na Mabadiliko hayo pamoja na kuzalisha kwa tija.
Sekta ya kilimo nchini ni Moja ya eneo ambalo limeadhiriwa na
Changamoto hiyo, kutokana na kupungua kwa mvua, ongezeko la ukame, kuongezeka
kwa wadudu washambuliao mazao pamoja na udongo kukosa rutuba ya kutosha.
Akizungumza na wakulima pamoja na Maafisa ugani Katika Skimu ya
Umwagiliaji ya Maliwanda Wilayani Bunda Mkoani Mara Mtafiti Uchumi na Jinsia
kutoka TARI Dkt.Theodore Kessy amesema ili wakulima wa zao la mpunga nchini
waweze kukabiliana na Changamoto hiyo wanashauliwa kutumia teknologia ya kilimo
Shadidi.
Dkt. Kessy ameongeza kuwa Kilimo shadidi kwenye zao la mpunga ni
teknologia ambayo upandikizwa miche michanga yenye umri kuanzia siku 8 hadi 14,
hupandwa mche mmoja kwenye shimo, kwa nafasi pana sentimeta 25 kwa 25 na mkulima
utakiwa kufanya palizi kwa kutumia vipalizi umwagiliaji wa kulowesha na
kukausha shamba, pamoja na kuweka mbolea.
Amesema kuwa teknologia hiyo ni Muhimu kwani Mkulima analazimika
kulima eneo dogo lakini ana uwezo wa kuvuna mazao mengi ikiwa atafuata kanuni
zote zinazotakiwa “ Kwenye hekari Moja mkulima anaweza vuna wastani wa mpaka
Tani 10 hi ni sawa na tani 4 kwenye ekari moja ya mpunga”
Naye Mtafiti na Mgunduzi kutoka TARI Dkt. Juliana Mwakasendo amebainisha
kuwa teknologia ya Kilimo Shadidi ni tofauti sana na kilimo cha kawaida, kwani
hakihitaji maji mengi, ambapo ameeleza Mkulima atatakiwa kuweka maji kwenye
shamba lake pale tu itakapohitajika kuwekwa maji.
" Tunajua kwenye kilimo cha kawaida cha zao hili wakulima
ugombania hadi maji maana kila mmoja uhitaji maji mengi, lakini Kilimo shadidi
Mkulima uhitaji maji kidogo, maji yanawekwa kwenye shamba pindi tu yanapokauka
ndipo mkulima anatakiwa kuweka mengine, siyo kila wakati shamba limejaa maji,”
ameeleza Dkt.Mwakasendo.
Amewashauri wakulima wa zao hilo nchini kubadilika na kuona kama
ni zao la kibiashara kwa kuacha kulima kwa mazoea, huku akisisitiza matumizi ya
teknologia hiyo itasaidia kuzalisha kwa tija, uwepo wa uhakika wa chakula,
kukua kwa pato la taifa na kuongeza ajira hasa Kwa vijana na akina mama.
TARI
inatekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wakulima na maafisa Ugani juu ya teknologia
ya kilimo shadidi kwenye zao la mpunga kupitia vituo vyake vya Uyole,
Ifakara na Mikocheni katika Wilaya za Mbarali, Iringa vijijini, Bunda vijijini,
Kilombero na Pwani.
Mradi
huo unaofadhiliwa na Norwegian Agency for Development Cooperation unalenga kuwajengea
uwezo wa Kitaasisi juu ya mifumo ya uzalishaji wa zao la mpunga
inayokuabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na rasilimali kwa ufanisi
kwa kuzingatia kilimo shadidi.
MWISHO.

Post a Comment