Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
Baraza la Madiwani la Hamashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu limepitisha Rasimu ya Mpango wa Bajeti kwa Mwaka 2024/25, kukusanya, kupokea na kutumia shilingi Bil. 31.
Akizungumza mwishoni mwa wiki jana kwenye kikao cha Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, David Masanja aliwataka Madiwani na Watendaji kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.
"Tumepitisha bajeti ya Bil. 31, wajibu wetu ni kuisimamia, kusimamia ukusanyaji wa mapato ushuru wa minada ya tozo mbalimbali ili tuweze kufikia malengo, pia wataalamu wasimamie miradi ikiwemo kupeleka fedha katika miradi ya maendeleo" Alisema Masanja.
Awali akiwasilisha Rasimu hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Adrian Jungu, Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Imelda Kirima alisema katika Bajeti ya 2024/25, Halmashauri hiyo inaomba kuidhinishiwa kukusanya, kupokea na kutumia jumla ya shlingi Bil. 31.
Alifafanua kuwa Makisio ya mapato ya ndani ni Shilingi Bil. 3.7, kati ya hizo mapato ya ndani bila vyanzo lindwa ni Shilingi Bil. 2.9 na mapato ya vyanzo lindwa ni shilingi Mil. 865.
Aliongeza kuwa matumizi mengine (OC) ni shilingi Mil. 923.6, mishahara shilingi Bil. 18.425, miradi ya maendeleo ufadhili wa nje shilingi Bil. 3.1 na fedha za maendeleo kwa ufadhili wa ndani shilingi Bil. 4.2.
Diwani wa kata ya Nyangokolwa Charles Nkenyenge aliwaomba watendaji wa kata na mitaa kusimamia ukusanyaji wa mapato ya mazao ya nafaka ikiwemo choroko ili kufikia lengo la bajeti bada ya wakulima kuzalisha mazao ya kilimo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Mwisho.
Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Imelda Kirima akiwasilisha Rasimu ya Mpango wa Bajeti ya mwaka 2024/25 katika kikao cha Baraza la Madiwani.
Post a Comment