Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Tri Yogo Jatmiko amefungua mafunzo ya utengenezaji viatu vya ngozi katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza, huku akiahidi mchango zaidi wa kujengeana uwezo katika sekta hiyo.
Mafunzo hayo yaliyokutanisha washiriki takribani 25 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania wakiwemo wajasiriamali wadogo, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ‘SSTC TVET Leather Footwear’ unaotekelezwa na Indonesia pamoja na Tanzania kuanzia mwaka 2022, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
Ni mafunzo ya siku 10 kuanzia Februari 26, yanayoendeshwa na wataalam wa masuala ya ngozi kutoka nchini Indonesia, ikiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania katika uzalishaji wa bidhaa za ngozi zenye viwango vya kimataifa.
“Tunahitaji Tanzania izalishe kiasi cha viatu vya ngozi kinachotosheleza mahitaji ya ndani kwa sababu mali ghafi zipo za kutosha, hatimaye iweze kuachana kabisa na uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje,” alisema Balozi.
Alisema serikali za nchi zote mbili zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu uliopelekea Marais wake kukutana mara mbili mwaka jana na kujadili masuala lukuki ya kimaendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo mafuta na kilimo.
Wakati huo huo, Balozi pia alipanda mti ikiwa ni uzinduzi wa ‘kampini ya kijani’ iliyolenga kuifanya Kampasi hiyo kuwa ya kijani, hivyo kuimarisha utunzaji mazingira.
Washiriki wa mafunzo hayo ya siku 10 kuanzia Februari 26, akiwemo Mwenyekiti wa kikundi cha ‘Umoja Leather’ cha jijini Mwanza, Trashishi Malibwa, alipongeza juhudi za Kampasi kuwaongezea ujuzi, hatua inayochochea ajira binafsi miongoni mwa wadau wa uchakataji ngozi.
Post a Comment