Na COSTANTINE MATHIAS, Busega.
MJUMBE wa Mkutano Mkuu Taifa (MNEC), kutoka Mkoa wa Simiyu, Gungu Silanga amekabidhi vitabu vya kanuni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Makatibu Kata wa mkoa huo ili waendelee kusimamia Utekelezaji wa Ilani ya chama hicho na kusimamia maadili ya Chama.
Aidha Gungu amewataka wanaCCM kuendelea kushikamana wakati huu wanaoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzo mkuu 2025.
Gungu aliyasema hayo jana kwenye Maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika katika kata ya Nyaluhande wilayani Busega Mkoani Simiyu ambapo alisema vitabu hivyo ni moja ya ahadi alizokuwa ameahidi kwa Makatibu hao.
‘’Niliahidi kutoa vitabu vya kanuni za CCM kwa Makatibu Kata, leo natimiza ahadi hiyo kwa kutoa vitabu 15 kwa Makatibu kata ya Busega kwa niaba ya wengine…hivyo nawaomba mkafanye kazi kwa kuzingatia miongozi na taratibu zilizomo kwenye kanuni, na Makatibu wengine watavichukua kwa Katibu wa CCM wa Mkoa’’ alisema Gungu.
Aidha Gungu aliwataka wanaCCM kutambua juhudi za Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye anaendelea kuchapa kazi za kuwatumikia Watanzania ambapo ametekeleza ahadi mbalimbali ikiwemo kuboresha huduma za Afya, Elimu, Maji na Umeme.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohamed alisema Chama Cha Mapinduzi kimefanya mambo makubwa katika nchi hii ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa huduma kijamii.
Aliwataka wanaCCM kuendelea kuunga mkono juhudi za Dk. Samia Suluhu Hassan huku akiwata Mabalozi kuhakikisha wanapita nyumba kwa nyumba ili CCM ishinde katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.
Kwenye Maadhimisho hayo CCM ilipokea wanachama wapya 50 waliopatiwa kadi za CCM pamoja na vijana wengine 50 waliopatiwa kadi za Umoja wa Vijana (UVCCM).
Aidha, Katika Maadhimisho hayo, Mwenyekiti Shemsa alichangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya CCM kata ya Nyaruhande, pia aliendesha harambee ambayo alifanikiwa kupata jumla ya mifuko 75 ya saruji na fedha kiasi cha shilingi 850,00/=.
MWISHO.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed (kushoto) akiwa katika picha ya Pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda (kulia), katika kati ni Mzee maarufu kutoka kata ya Nyaruhande.
Post a Comment