Taarifa kwa vyombo vya habari | 16 February 2024
Nusu ya waandishi wa habari nchini Tanzania wameripoti kutishwa au kunyanyaswa
wakiwa kazini.
Tarehe 16 Februari 2024, Dar es Salaam: Nusu (50%) ya waandishi wa habari nchini Tanzania wameripoti
kukumbana na vitisho, manyanyaso, mateso au kushambuliwa katika kazi zao. Wawili kati ya kumi (22%)
wamekamatwa au kuzuiliwa na mamlaka, na idadi sawa na hiyo wamekumbana na unyanyasaji wa kijinsia
(20%) au kunyang’anywa vifaa vyao vya kazi (20%).
Twaweza ikishirikiana na MISA-TAN, Jamii Forums, UTPC na TAMWA wametoa matokeo haya kwenye jarida
la utafiti lenye kichwa cha habari Sautiza Waandishi: Uzoefu na maoni ya waandishi wa habari wa Tanzania.
Jarida hili linawasilisha takwimu kuhusu uzoefu na maoni ya waandishi wa habari wa Tanzania.
Maoni yalikusanywa kutoka kwa kwa wanahabari 1,202 wakiwemo waandishi wa habari, wahariri na
wanablogu.
Wanahabari hawa wamepatikana kutokana na kanzidata za uanachama wa vyama
mbalimbali vya vyombo vya habari ambavyo ni Chama cha Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC),
Chama cha Wanawake Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa
Afrika Tawi la Tanzania (MISA-Tan) na Jamii Forums.
Mahojiano yalifanyika kwa njia ya simu kati ya
Septemba 23 na Novemba 7, 2023.
Waandishi wengi wa habari wana ajira zisizo za kudumu, na zisizo za uhakika. Wawili kati ya kumi (20%)
wanataja kuwa ajira zao ni za kudumu, ikilinganishwa na sita kati ya kumi (60%) wanaosema ni za muda na
wawili kati ya kumi (18%) wanaosema wanaitwa kazini pale tu wanapohitajika.
Nusu (50%) wanayo
mikataba iliyosainiwa. Waandishi wengi wa habari (63%) wanasema ni vigumu kujipatia kipato kinachokidhi
mahitaji muhimu kupitia uandishi wa habari, wakati wachache (5%) wanasema si tatizo. Mmoja kati ya
waandishi watatu (36%) wana kazi nyingine inayowalipa mbali na kazi yao ya uandishi.
Ni wanahabari wawili
kati ya kumi (19%) tu ndio wangependelea watoto wao wafuate nyayo zao kuwa waandishi wa habari.
Uzoefu wa waandishi wa habari kuhusu hatari wakiwa kazini ni mkubwa. Nusu (50%) wanaripoti kwamba
wamewahi kutishiwa, kuteswa au kushambuliwa wakiwa kazini.
Waandishi wa habari kwa kiasi kikubwa
wanawatuhumu maafisa wa serikali kama chanzo kikuu cha vitisho; zaidi ya nusu (56%) wanasema maafisa
wa serikali ni chanzo kikuu cha vitisho, zaidi ya kundi lingine lolote.
Wanahabari walio wengi (86%) wanasema rushwa ipo katika sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na 36% wanaosema
rushwa ipo kwa kiwango kikubwa. Aina za rushwa zilizokithiri ni malipo kwa ajili ya kuchapisha (55%) au
kutokuchapisha (53%) habari fulani.
Karibu wote (95%) wanasema wanakubali pesa kutoka kwa watu au
taasisi zinazohusika na Habari, (23%) wanakubali mara kwa mara, na (72%) wameshakubali mara kadhaa.
Mmoja kati ya kumi (10%) anaripoti kupokea ‘mara zote’ zawadi au pesa ili kubadilisha maudhui, na nusu
(53%) wanasema wameshafanya hivyo angalau mara moja.
Aidha, waandishi wa habari wanahisi kwamba vyombo vya habari nchini Tanzania vina uhuru mdogo wa
kufanya kazi bila kudhibitiwa au kuingiliwa. Wanahabari sita kati ya kumi hawajisikii huru kuripoti kuhusu
rushwa (60%) au masuala yanayohusiana na vyombo vya ulinzi na usalama (61%).
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, alisema: "Waandishi wa Habari wana majukumu
muhimu sana nchini, yakiwemo kuwataarifu, kuwaelimisha na kuwaburudisha wananchi, pamoja na
kuwawajibisha waliopo madarakani. Lakini mazingira wanayofanyia kazi si rafiki. Wanakutana na vitisho
na unyanyasaji kwa sababu tu ya kusaka na kutangaza ukweli. Kipato cha walio wengi sio cha kutegemea,
na hakikidhi mahitaji yao muhimu.
“Wanahabari wanayo haki ya kulindwa dhidi ya vitisho na unyanyasaji. Wanastahili kuwa na mikataba ya
kazi na yenye maslahi mazuri. Sheria ziwalinde wanahabari, badala ya kuwatisha ili wasiibue ukweli. Nafasi
ya waandishi wa habari katika jamii ni muhimu; sisi sote tunapaswa kufanya kila tuwezalo kuwalinda na
kuwastawisha.”
---- Tamati ----
Kwa taarifa zaidi wasiliana na: Annastazia Rugaba | e: arugaba@twaweza.org | t: (+255) (0)687 222 197
Maelezo kwa Wahariri
Jarida hili na takwimu zake zinapatikana: www.twaweza.org
Twaweza inafanya kazi kupitia tafiti, ushahidi na kuchukua hatua ili kuonesha jinsi ambavyo wananchi
wanaweza kushirikiana kutatua matatizo yao na kuifanya serikali iwajibike vizuri zaidi kwa wananchi;
kuwezesha wananchi kupaza sauti zao kwenye masuala yanayohusu maslahi na uzoefu wao ili yasikilizwe
na kuzingatiwa wakati wa kufanya maamuzi; na inahimiza kuweka mazingira wezeshi kwa ushirikishwaji wa
wananchi na serikali kuitikia mahitaji ya wananchi nchini Tanzania, Kenya na Uganda. Tufuatilie kwenye
Twaweza Tanzania (Facebook), @Twaweza_NiSisi (Twitter) na @Twaweza_EastAfrica (Instagram).
TAZAMA VIDEO HAPA
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment