Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, Shinyanga, Mwl. Paschal Shiluka akizungumza kwenye mahafali ya 12.
Na Elisha Shambiti - Misalaba Media
Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, Shinyanga, Mwl. Paschal Shiluka, amewataka wahitimu wa kozi za afya katika chuo hicho wasiifanye elimu waliyoipata kuwa mali yao bali kuwa mali ya jamii ili kuweza kuisaidia jamii zao kuondokana na changamoto mbalimbali zinazohusiana na afya.
Katika hotuba yake kwenye mahafali ya kumi na mbili (12) ya chuo hicho yaliyofanyika Ijumaa, Mwl. Shiluka alisema kuwa wahitimu wanapaswa kutumia elimu waliyoipata kuzigeuza changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii zao kuwa fursa ambazo zitawaletea maendeleo binafsi na kwa taifa kwa ujumla.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo hicho, Dk. Luzila John, amewataka wahitimu hao kwenda kuwa mabalozi wema wa chuo hicho katika jamii zao kwa kuzingatia maadili mema, kwani elimu na taaluma bila maadili si kitu chochote.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT), Mch. Mwl. Josephales Mtebe, amesema kuwa wahitimu wanapoenda kufanyia kazi taaluma zao wanapaswa kuonyesha upendo na ukarimu kwa wagonjwa, jambo litakalosaidia wagonjwa kupata nafuu kabla ya kupatiwa matibabu mengine.
Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Christina Mzava, ambaye alimuwakilisha mgeni rasmi Naibu Waziri ofisi ya waziri mkuu kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Mhe. Paschal Patrobas Katambi, katika mahafali hayo, amesema kuwa wahitimu wanapaswa kujua kuwa serikali haiwezi kuwaajiri vijana wote wanaohitimu masomo yao na badala yake wajifunze kujitegemea wenyewe kwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo kwenye jamii zao kama vile kutumia fursa za mikopo kwa makundi ya vijana ambayo imekuwa ikitolewa na serikali.
Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto kinachomilikiwa na Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) kilianzishwa mwaka 1957 kikianza na udahili wa wanafunzi kumi na mbili ambapo Agosti 2,2024 jumla ya wanachuo 316 wamehitimu mafunzo yao kutoka kozi za maabara ya viwanda, uuguzi na ukunga, maabara ya binadamu, utabibu na famasia.
Mgeni rasmi, Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Christina Mzava akizungumza kwenye mahafali ya 12 katika chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto Agosti 2,2024.
Katibu Mkuu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT), Mch. Mwl. Josephales Mtebe, akizungumza kwenye mahafali ya 12 katika chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto Agosti 2,2024.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo hicho, Dk. Luzila John, akizungumza kwenye mahafali ya 12 katika chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto Agosti 2,2024.
Post a Comment