Meneja wa TCRA Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Francis Mihayo
Meneja wa TCRA Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Francis Mihayo
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Francis Mihayo, ameendelea kupaza sauti kuhusu kampeni ya "Ni Rahisi Sana" ambayo ina lengo la kuhamasisha Watanzania wote kuhusu usalama mtandaoni.
Mhandisi Mihayo ameshiriki katika vipindi vya redio katika Vituo vya Redio mbalimbali Mkoani Kilimanjaro ikiwemo Moshi FM, Tanakh FM ,Shine FM ,Galaxy FM na Peak Media kwa ajili ya kutoa elimu hiyo.
Katika mahojiano yaliyofanyika katika vituo hivyo vya redio, Mhandisi Mihayo ameelezea jinsi ambavyo mazingira salama mtandaoni yatasaidia kufikia malengo ya uchumi wa Kidijitali nchini.
Mhandisi Mihayo amesema TCRA inaendelea kutoa elimu kuhusu jinsi ya kujilinda dhidi ya uhalifu mtandaoni, ikiwa ni pamoja na kugundua udanganyifu, kulinda taarifa za kibinafsi, na kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia.
Amesema Kampeni ya "Ni Rahisi Sana" inaendelea kuhamasisha wananchi kuhusu hatari zinazoweza kutokea mtandaoni na jinsi ya kujilinda dhidi ya udukuzi na udanganyifu.
"Hii ni sehemu ya juhudi za Mamlaka ya Mawasiliano ya Tanzania (TCRA) kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu ya kutosha kuhusu usalama mtandaoni. Kampeni hii inasisitiza kuwa ni rahisi sana kutambua tapeli, kutoa taarifa za udukuzi, kuwasiliana na TCRA, na kuchukua hatua za tahadhari mtandaoni. Pia, inasisitiza umuhimu wa elimu ya kidijitali kwa watoto na vijana, na kuwawezesha wananchi kufanya biashara salama mtandaoni",amesema.
KUHUSU UDUKUZI
Mhandisi Mihayo, ametumia fursa hiyo kuwatahadharisha watumiaji wa mitandao ya kijamii kuhusu wimbi la udukuzi ambalo limekuwa likishika kasi, ambapo wahalifu wamekuwa wakivamia akaunti za Facebook na WhatsApp.
Mhandisi Mihayo amesema kuwa wahalifu hutumia mbinu mbalimbali kuiba akaunti za watu, kisha kuanza kusambaza viunganisho (links) vya udukuzi au kuomba fedha kwa njia ya udanganyifu.
"Ni muhimu kuwa makini na viunganisho unavyobofya kwenye mitandao ya kijamii, hasa kutoka kwa watu usiowajua. Hii inaweza kuwa ishara ya kuingiliwa kwenye akaunti yako," amesema Mhandisi Mihayo.
Amesisitiza kuwa endapo mtumiaji atabaini kuwa akaunti yake imevamiwa (hacked), ni muhimu kutoa taarifa haraka katika kituo cha polisi ili kuchukua hatua za kurejesha usalama na kuzuia madhara zaidi.
"Ikiwa umebaini kwamba akaunti yako imevamiwa, usichelewe kutoa taarifa polisi ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa. Usalama wa taarifa zako za kifedha na binafsi ni muhimu sana," ameongeza.
"Epuka Kubofya Viunganisho Visivyokuwa na Uhakika: Usikubali kubofya viunganisho (links) vinavyotumwa na watu usiowajua au visivyokuwa na maelezo ya kina. Usifuate Maelekezo ya Watu Usiowajua: Ikiwa mtu anakuambia ufanye jambo fulani mtandaoni, hakikisha kwamba anajulikana kwako na kuwa na nia nzuri".
"Jiridhishe na Unaye - Chat naye (unayewasiliana naye) hakikisha kabla ya kufanya jambo lolote la kifedha au kuungana na mtu mtandaoni, hakikisha ni mhusika unayemjua. Usitumie pesa kwa watu usiowajua na hakikisha kila wakati kuwa maombi ya kifedha ni halali na jiridhishe na usitumie wala usitume namba za uthibitisho (codes) ambazo unazipokea mtandaoni au kwenye kifaa chako cha mawasiliano mfano simu au Kompyuta, hasa kutoka kwa watu usiowajua, kwani inaweza kuwa mbinu ya Mdukuzi kuiba taarifa zako na kudukua akaunti ya Whatsapp au Facebook",ameeleza Mhandisi Mihayo.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment