AFISA Ugani wa Kampuni ya Alliance Ginnery kupitia Mradi wa Jenga Kesho Bora (BBT), Kijiji cha Nyanguge, Leah John, akitoa Elimu ya Kudhibiti Wadudu wa pamba mbele ya waandishi wa habari. (Picha na Costantine Mathias).
WAKULIMA wa Pamba wilayani Bariadi Mkoani Simiyu wametakiwa kuzingatia Ushauri na maelekezo ya Maafisa Ugani katika kutunza mashamba yao hasa kipindi hiki cha kudhibiti wadudu ili waweze kuvuna kwa tija na kupata mazao mengi.
Aidha, Wakulima hao wameaswa kukagua mashamba yao mara kwa mara huku wakiwashirikisha Wataalamu wa kilimo ili waweze kuwaibini wadudu wanaoshambulia vitumba vya Pamba kwa lengo la kudhibiti wadudu wanaofyonza na kutafuna Pamba.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Afisa Ugani wa Kampuni ya Alliance Ginnery kupitia Mradi wa Jenga Kesho Bora (BBT), Kijiji cha Nyanguge, Leah John amesema awali wakulima hawakuwa na Elimu ya kukagua na kutambua wadudu marafiki na wadudu maadui wa Pamba shambani.
"Tunafundisha wakulima kukagua wadudu aina ya Chawa Jani ambao wanakaa nyuma ya Jani, vitumba vikitoka tunawaambia wakulima wakague vipepeo nondo wanaosababisha funza...tuna mitego ya Molasisi ambayo tunaigawa wakulima ili waweze kudhibi wadudu wanaoshambulia Pamba" amesema.
Ameongeza kuwa kutokana na Elimu wanayopatiwa wakulima wa Pamba, wamefundishwa namna sahihi ya kunyunyizia dawa mashambani kuanzia chini ya majani kuelekea juu.
Marco Kubagwa, Mkulima wa Pamba kutoka kijij Cha Nyanguge, amesema Maafisa Ugani hao wameimarisha huduma za Ugani vijijini na kwamba wakulima wanatembelewa mashambani na kupewa elimu mara kwa mara.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imesambaza Maafisa Ugani vijijini kupitia Mpango wa Jengo Kesho Bora (BBT) ili washirikiane na Maafisa Kilimo wa serikali kumhudumia, kumwelimisha na kumfikia kila wakati mkulima ili aweze kuzalisha kwa tija.
Mwisho.
Post a Comment