BIL. 100 KUMALIZA KERO YA MAJI TUNDUMA






Na Moses Ng'wat, Tunduma.


Serikali ya Awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imechukua hatua thabiti kumaliza changamoto ya maji katika  Mjini wa Tunduma , Wilayani Momba, Mkoa wa Somgwe kwa kutenga shilingi bilioni 100 kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji.


Akizungumza katika ukumbi wa High Class Tunduma mnamo Februari 22, 2025, wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Momba, Fadhiri Maganya, Mbunge wa Tunduma na Naibu Waziri wa Maji, David Silinde, alieleza kuwa mradi huo utaimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Tunduma.


“Tayari shilingi bilioni 38 zimeshatolewa na Rais Samia kwa hatua za awali za utekelezaji wa mradi huu na mwezi ujao, Waziri wa Maji, Juma Aweso, pamoja na Waziri wa Fedha, wanatarajia kufika Tunduma kumkabidhi mkandarasi ili aanze kazi rasmi,” alisema Silinde huku akishangiliwa na wananchi na wanachama wa CCM waliohudhuria mkutano huo.


Kwa miaka mingi, wakazi wa Tunduma wamekumbwa na uhaba wa maji, hali iliyokuwa ikiathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.


Hata hivyo, juhudi hizi mpya za Serikali zinatoa matumaini kwa wananchi, huku viongozi wa chama na Serikali wakiahidi kuwa mradi huo utaleta maendeleo endelevu katika eneo hilo.


Mwisho.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post