Na Philipo Hassan - Tanga


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kiwango cha lami barabara inayounganisha Tanga, Pangani, Saadani na Bagamoyo pamoja na Daraja la Mto Pangani lenye urefu wa mita 525 zitasaidia kuifungua Tanga Kiutalii na kiuchumi.


Rais Samia ameyasema hayo leo, Februari 26, 2025 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa  barabara na Daraja la Mto Pangani ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara yake mkoani Tanga. Vilevile, alisisitiza kuwa miundombinu hiyo mipya itarahisisha maeneo mengi ya utalii kufikika kiurahisi.


Rais Samia alieza “Barabara hii tunayoiunganisha inaenda kuifungua Tanga kiutalii na kibiashara. Maeneo mbalimbali ya kiutalii ambayo hayafikiki, itakuwa ni rahisi kumtoa mtalii Hifadhi ya Taifa Saadani na kwenda kutalii maeneo mengine ndani ya Mkoa wa Tanga” 


Naye, Mbuge wa jimbo la Pangani Mhe. Jumaa Aweso alimshukuru Rais Samia kwa kutekeleza mradi mkubwa wa barabara na Daraja ambayo yatachochea maendeleo ya kiuchumi ndani ya Wilaya ya Pangani.


“Barabara hii ya Tanga, Pangani, Saadani na Bagamoyo itachochea uwekezaji ukizingatia 

Pangani tuna Hifadhi ya Taifa Saadani, Hifadhi pekee inayopakana na Bahari ya Hindi. Tukipata “Fast Boat” shida ya usafirishaji itaisha na watalii watapita kutoka Zanzibar kuja kutembelea Saadani” alisema Mhe. Awesu.


Hifadhi ya Taifa Saadani ni moja kati ya Hifadhi za Taifa 21 Tanzania yenye upekee wake wa mandhari ya nyika kukutana na  bahari katika eneo moja ambapo ni kivutio kikubwa cha utalii kwa ukanda wa pwani.


Ziara hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) pamoja na wakuu wa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii akiwemo Kamishna wa Uhifadhi TANAPA.