TANESCO SONGWE YAELEZA SABABU ZA KUKATIKA KWA UMEME MARA KWA MARA.



MKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo.


Na Moses Ng'wat, Songwe


SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa ufafanuzi kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara katika Mkoa wa Songwe, tatizo ambalo limekuwa kero kwa wananchi kwa muda mrefu.


Meneja wa TANESCO Mkoa wa Songwe, Mhandisi Tumaini Chonya, alitoa maelezo hayo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, kutaka ufafanuzi kuhusu changamoto hiyo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika leo, Februari 20, 2025, katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.


Akizungumzia hali hiyo, Mhandisi Chonya alisema tatizo linatokana na kiwango cha chini cha umeme (low voltage), lakini TANESCO imechukua hatua za kulitatua kwa kubadilisha nyaya kutoka kituo kidogo cha kupooza umeme cha Karasha wilayani Mbozi hadi kituo kikuu cha kupooza umeme cha Mwakibete, Mbeya, umbali wa kilomita 100.


"Naomba niwajulishe kuwa tumekuwa tukifanya kazi ya kubadilisha nyaya kwa muda mrefu. Changamoto kubwa ni hali ya hewa ya mvua zinazoendelea kunyesha pamoja na mashamba ya wananchi , hivyo kutufanya tushindwe kusafirisha vifaa kwa urahisi kwa kutumia magari kwa hofu ya kuharibu mazao yaliyopo" alisema Chonya.


Hata hivyo, aliahidi kuwa tatizo hilo litapatiwa suluhisho ifikapo kesho, Februari 21, 2025 kwa kuwa kipande kidogo kilichobaki kufika katika kituo kikuu cha kupooza umeme cha Mwakibete  kitakamilika kesho na kwamba hali hiyo ya kukatika itakua imekoma.


 Aidha, Mhandisi Chonya aliwaomba radhi wajumbe wa kikao na wananchi wa Songwe kwa usumbufu uliojitokeza.


Akifunga kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, alimtaka Mhandisi Chonya kutoa maelezo ya kina kuhusu hali hiyo ya kukatika kwa umeme mara kwa mara na kuhakikisha tatizo hilo linashughulikiwa kwa haraka.


Wananchi wa Songwe wameendelea kulalamikia kukatika kwa umeme, hali inayosababisha athari kwa shughuli zao za kiuchumi na kijamii. Mkoa wa Songwe ni miongoni mwa mikoa yenye viwanda vingi, hasa katika miji ya Mlowo na Kamsamba, ambako mahitaji ya umeme ni makubwa kwa ajili ya kuchakata bidhaa za kilimo. Pia, mji wa mpakani wa Tunduma una shughuli nyingi za kiuchumi zinazohitaji umeme wa kutosha.


Mwisho.







Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post