Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetangaza mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake ni pamoja na serikali kuongeza uwekezaji katika ujenzi wa vyuo kutoka Sh.bilioni 116 hadi kufikia Sh.bilioni 516 hivi sasa.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya miaka 30 ya utoaji na utekelezaji wa shughuli za mafunzo ya ufundi stadi hapa nchini na miaka 50 ya utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Alisema VETA ilipoanzishwa 1994 kulikuwa na vyuo 14 lakini leo vipo 80 katika mikoa na wilaya nchini wakati vyuo binafsi vinavyomilikiwa na taasisi na mashirika vimeongezeka kutoka 50 hadi kufikia zaidi ya 770 na hivyo kufanya nchi nzima kuwa na jumla ya vyuo 870.
Kasore alisema ongezeko hilo la vyuo limesababisha kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi kufikia 380,000 kutoka 38,360 waliokuwa wakidahiliwa mwaka 1994.
"Mwaka 1994 wakati VETA ilipokuwa na vyuo 14 ilikuwa na uwezo wa kuchukua wananchi 1,940 kuwapatia mafunzo mbalimbali katika vyuo vyake lakini sasa wanachukuliwa wananchi 83,900 ambao wanapewa mafunzo na hivyo kushiriki shughuli za uzalishaji mali,"alisema.
Mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi hicho ni ongezeko la watoto wa kike wanaochukuliwa katika vyuo vya VETA ambao wamefikia 150,000 kutoka 4600 waliokuwa wanachukuliwa mwaka 1994.
Kasore aliongeza kuwa hivi sasa vinajengwa vyuo vingine vipya 65, kati ya hivyo kimoja cha hadhi ya mkoa kinajengwa Mkoa wa Songwe na 64 katika wilaya mbalimbali nchini ambapo serikali imeshatoa Sh.bilioni 100 na vitakapokamilika vitafanya idadi ya vyuo vinavyomilikiwa na VETA kufikia 145.
Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo, alisema yatafanyika katika ngazi ya vyuo na kanda mbalimbali kote nchini na kilele kitaadhimishwa kwa siku nne kuanzia Machi 8 hadi 21, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Alisema maadhimisho haya yana lengo la kutambua na kusherehekea mchango wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika maendeleo ya taifa,kutathimini mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizojitokeza na kujadili mwelekeo wa sekta ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa kipindi hicho kwa kuzingatia sera ya elimu ya mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023.
Kasore alisema wakati wa maadhimisho hayo shughuli zitakazofanyika ni maonesho ya kazi,ubunifu wa teknolojia kutoka kwenye vyuo vya ufundi stadi na wadau wake na programu za mafunzo na huduma zinazotolewa na VETA
"Wakati wa maadhimisho kutakuwa na mashindano ya ujuzi yatakayowashirikisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kuonesha umahiri katika katika stadi mbalimbali,"alisema.
Aliongeza kuwa pia kutafanyika kongamano la wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kujadili mambo mbalimbali na utoaji wa tuzo kwa taasisi,wadau na wahitimu waliochangia katika maendeleo ya sekta ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi hapa nchini.
MWISHO.
Post a Comment