Na Mwandishi Maalum.
Ikiwa leo wanawake wa Tanzania wanaungana na wenzao kote ulimwenguni kuadhimisha kilele cha siku ya wanawake duniani, ni vema tukakumbuka mchango wa Mama Magreth Manoni (75) mwanamke pekee kutoka Shinyanga aliyeshiriki harakati za kimataifa katika kupigania haki za wanawake.
Mwanamama huyu ambaye kwa sasa anaishi Mwasele katika Manispaa ya Shinyanga, ameshiriki mikutano mikubwa ya kimataifa iliyokuwa ikijadili juu ya kumkomboa mwanamke, ambayo ni pamoja na Mkutano wa nne wa Jukwaa la wanawake duniani uliofanyika mwaka 1995 Beijing nchini China na mwingine uliofanyika mnamo mwaka 2001 nchini Marekani.
Ushiriki wake kwenye mikutano hiyo umechangia kwa kiwango kikubwa kuchochea mabadiliko ya kijamii ambayo tunayashuhudia hivi sasa, yaliyoleta nafuu kwa wanawake wa mkoa wa Shinyanga.
Ni mwanzilishi mwenza wa shirika la Msaada wa sheria kwa wanawake na watoto la Paralegal Aid Centre Shinyanga (PACESH) ambalo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, limekuwa msaada mkubwa kwa mamia ya wanawake wa Shinyanga kwa kuwaelimisha kujua haki zao na kuwasaidia kupata haki kwenye vyombo vya sheria.
HISTORIA YAKE
Mama Magreth Manoni ambaye ni Mama wa watoto wanne wote wakiwa ni wa kiume, alizaliwa mnamo mwaka 1950 katika kijiji cha Luguru Wilayani Bariadi mkoani Simiyu, ambapo zamani ilikuwa sehemu ya mkoa wa Shinyanga kabla ya kuanzishwa kwa mkoa wa Simiyu mwaka 2012.
Wazazi wake licha ya kwamba walikuwa wafugaji na wakulima, walitambua umuhimu na thamani ya kumsomesha mtoto wa kike , ambapo mwaka 1959 walimwandikisha kuanza darasa la kwanza katika shule ya msingi Luguru, ambako alisoma hadi darasa la nne na kuhitimu mwaka 1962.
Mama Manoni alikuwa ni mwanafunzi pekee aliyefaulu kuendelea na shule ya kati (Middle school) katika wilaya ya Maswa iliyokuwa inajumuisha eneo lote la wilaya za Bariadi na Meatu, ambapo alichaguliwa kujiunga na shule ya St. Mary’s Middle School mjini Shinyanga iliyokuwa ikisimamiwa na watawa wa Kanisa Katoliki, ambayo kwa sasa ni Shule ya Msingi Buhangija.
Alisoma St.Mary’s Middle school katika kipindi cha miaka mitatu kati ya mwaka 1963 na mwaka 1965, baada ya kuvukishwa darasa moja kutokana na uwezo wake darasani.
Baada ya kuhitimu elimu ya kati, alifaulu na kuchaguliwa kujiunga na shule ya Sekondari Rozaly iliyopo mkoani Mwanza (kwa sasa Shule ya Sekondari Nganza) ambapo alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne kuanzia mwaka 1966 hadi mwaka 1969.
Alipomaliza elimu ya Sekondari, mwaka 1970 alijiunga na Jeshi la kujenga taifa (JKT) na baadaye alijiunga katika chuo cha ualimu Kigurenyembe kilichopo mjini Morogoro, ambako alihitimu mwaka 1971.
Aliporudi Shinyanga aliajiriwa kama Mwalimu katika mgodi wa Mwadui na kufundisha shule ya msingi Mwadui kati ya mwaka 1972 hadi mwaka 1984 alipohamishiwa katika shule ya msingi Mwenge mjini Shinyanga ambapo alifanya kazi miezi michache na baadaye mwanzoni mwa mwaka 1985 akahamishiwa katika shule ya msingi Bugoyi ya mjini Shinyanga kwenda kuwa Mwalimu mkuu wa Shule hiyo.
Mwaka 1987 alipandishwa cheo na kuwa Mratibu wa Elimu Kata na kufanya kazi katika Kata za Ngokolo, Chamaguha, Mjini, Ibinzamata na Kizumbi mpaka alipostaafu mwaka 2010.
HARAKATI ZA KUPIGANIA UKOMBOZI WA MWANAMKE
Ikumbukwe kuwa, Mwanamama huyu akiwa Mwalimu alijiendeleza kielimu na kuwa mbobevu katika masuala ya Siasa na Lugha za Kiswahili na Kiingereza, hatua ambayo ilimwezesha kupata fursa mbalimbali ikiwemo kuwa mjumbe aliyeuwakilisha mkoa wa Shinyanga katika Baraza la wanawake Tanzania (BAWATA) ambalo wakati huo Mwenyekiti wake alikuwa Profesa Anna Tibaijuka.
Baada ya kuitishwa kwa Mkutano wa nne wa jukwaa la wanawake duniani uliofanyika mwaka 1995 huko Beijing nchini China, Mama Manoni alikuwa miongoni mwa wanawake walioiwakilisha Tanzania kwenye Mkutano huo akiwa ameambatana na wanawake mashuhuri wakiwemo akina Profesa Anna Tibaijuka, Anna Makinda na Getrude Mwongela ambaye alichaguliwa kuwa Katibu wa Mkutano huo, uliolenga kujadili namna ya kumkwamua mwanamke, ukiwa na Ajenda 12 zilizogusa moja kwa moja maslahi ya wanawake ambazo ni pamoja na Elimu, Afya, Umaskini, Athari za vita, maendeleo, Sera za kiuchumi, Mazingira, vyombo vya Habari, ukatili wa kijinsia, siasa na ushirikishwaji katika ngazi za maamuzi.
MATOKEO YA MKUTANO HUO KWA WANAWAKE WA SHINYANGA
Mkutano wanne wa wa jukwaa la wanawake duniani ndiyo unatajwa kuchochea vuguvugu la ukombozi kwa mwanamke nchini Tanzania na kuleta mabadiliko makubwa katika usawa wa kijinsia ambayo yanashuhudiwa hivi sasa.
Mama Manoni ambaye alikuwa ni Mwanamke pekee kutoka katika mkoa wa Shinyanga aliyehudhuria mkutano huo, alifikiria namna ya kutumia maarifa aliyoyapata kutatua changamoto za manyanyaso na ukandamizaji mkubwa wa kijinsia ambao walikuwa wanakumbana nao wanawake wa Shinyanga, kutokana na mfumo dume uliorithiwa na jamii toka enzi za mababu.
Wakati huo mkoa wa Shinyanga ulikuwa kati ya mikoa iliyokuwa ikiongoza nchini kwa vitendo vya ukatili kwa wanawake ikiwemo mauaji ya wanawake vikongwe kwa imani za kishirikina, watoto wa kike kulazimishwa kuolewa katika umri mdogo na kunyimwa fursa ya kupata elimu, vipigo, wanawake kunyang’anywa mali pindi waume zao wanapofariki na kunyimwa fursa mbalimbali za kiuchumi.
Hali hiyo ilimpa wazo la kuanzisha chombo maalum cha kubadilisha mtazamo wa jamii na kuwasaidia wanawake wa Shinyanga kisheria ili kutetea haki zao ambazo walipokonywa kwa muda mrefu.
Alitumia maarifa aliyoyapata kuwashawishi wanawake wenzake akiwemo Mama Pelepetua Magoke ambaye pia alikuwa Mwalimu, ambapo mwaka 1996 wakafanikiwa kuanzisha shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la Paralegal Aid Centre Shinyanga (PACESH) chini ya ulezi wa Shirika la Women’s Legal Aid Centre (WLAC) la jijini Dar es Salaam, hatua ambayo ilifikiwa baada ya kufanikiwa kumshawishi aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika hilo Mama Monica Mhoja ambaye pia ni mzaliwa wa mkoa wa Shinyanga.
Shirika la PACESH ambalo ni la kwanza katika kutoa msaada wa sheria mkoani Shinyanga, limekuwa kimbilio kwa wanawake na jamii katika kupata usaidizi pale wanapodhulumiwa haki zao, linatoa elimu ya kisheria, kijinsia na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.
Shirika la PACESH pia linatoa ushauri na msaada wa kufungua kesi Mahakamani ikiwemo kugharamia Mawakili wa kuwatetea Mahakamani wanawake wasiokuwa na uwezo.
Shirika la PACESH tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, linatajwa kuwahudumia moja kwa moja wanawake zaidi ya Elfu sita kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga.
MAMBO AMBAYO MAMA MANONI ANAJIVUNIA
Mama Manoni anajivunia kuona wanawake wengi wa mkoa wa Shinyanga sasa wanatambua haki zao na namna ya kuzidai.
Mabadiliko ya kifikra na kijamii ambayo yamesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza vitendo vya kwa ukatili wa kijinsia.
Shirika la PACESH kuzidi kupata washirika wanaosaidia kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya ukandamizaji wa wanawake na watoto hali kadhalika wanawake wa Shinyanga kuwa na chombo wanachoweza kukikimbilia kupata msaada pale wanapohisi kudhulumiwa haki zao.
USHAURI WAKE KWA WANAWAKE
Waendelee kutambua nafasi yao katika jamii na kutorudi nyuma katika juhudi za kujikomboa na wawe na umoja katika kupigania haki zao.
KUHUSU KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI
Mama Manoni ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi balimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu na kwamba, vikwazo walivyokuwa wakivihofia vimepungua kwa kiwango kikubwa.
Amewaomba wanawake wanaoshika hatamu za uongozi kuwa mfano wa kuigwa pale wanapopewa fursa ili kujenga imani kwa jamii hatua ambayo itawafanya waaminike na kuwavuta wenzao ambao bado wanahofu kujitosa katika kugombea.
Amewashauri wanawake kuacha wivu, kupinga rushwa na kuwaunga mkono wenzao wanaogombea nafasi mbalimbali ili kupata wawakilishi katika ngazi za maamuzi ambao wanafahamu changamoto zinazowakabili.
WITO WAKE KWA SERIKALI NA TUME YA UCHAGUZI
Waondoe viti maalum Bungeni ili sasa wanawake wasimame na kugombea wenyewe badala ya kusubiri hisani ya viti maalum hatua ambayo anaamini inawafanya waendelee kubweteka licha ya kuwezeshwa vya kutosha.
Rushwa na matumizi ya fedha nyingi kwenye uchaguzi vikomeshwe kwa sababu hali hiyo bado inaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake kupenya kwenye siasa kutokana na hali zao kiuchumi.
Pia ameitaja rushwa ya ngono kuwa bado ipo na imekuwa kikwazo kikubwa katika harakati za wanawake kujikwamua kwa vile ni ngumu kuithibitisha mahakamani kwa sababu inaombwa katika mazingira ya siri.
AMPONGEZA RAIS DKT.SAMIA SULUHU HASSAN
Mama Manoni amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambazo anazifanya hatua ambayo imewaheshimisha wanawake na kuonyesha kuwa wakipewa nafasi wanaweza.
Ametumia nafasi hiyo kuwaomba watanzania waendelee kumuunga mkono kwa kumpigia kura kwenye uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
Mwisho.

Post a Comment