DARAJA LA MTO NGASHANDA KUNUSURU MAISHA YA WANANCHI KATA TATU BARIADI.

 

Daraja la mto Ngashanda katika halamshauri ya Mji wa Bariadi lililowekewa jiwe la msingi na Mbio za Mwenge Kitaifa 2025.


Na Samwel Mwanga, Bariadi.


WAKAZI  wa Kata za Malambo, Nyangokolwa na Somanda katika halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu wataepuka hatari ya kupoteza maisha baada ya daraja jipya kumalizika kujengwa katika Mto Ngashanda.



Daraja hilo ambalo limekamilika kwa asilimia 100, limezinduliwa leo Jumanne, Agosti 12, 2025 na kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2025, Ismail Ussi alipokwenda kutembelea mradi huo uliojengwa na serikali ambapo ujenzi wake umegharimu Sh 1.3 bilioni.



Editha Daud ni mkazi wa Ngashada amesema kuwa wananchi wa eneo hilo wamepata madhara mbalimbali ikiwemo kutumbukia mtoni, kujeruhiwa na wengine kupoteza maisha mtoni hapo.



“Kukamilika kwa daraja hili ni mkombozi kwa wananchi ambao tunalitumia kwani hapo awali tulikuwa tunapa madhara mbalimbali ikiwemo wanafunzi kukosa masomo kwa muda wa siku mbili mto unapokuwa unajaa na wengine kutumbukia mtoni,”



“Tunaishukuru sana kusema ukweli tumepitia changamoto mbalimbali wanafunzi wanashindwa kufika kwa muda muafaka shuleni kutokana na mto kujaa,mimi ni miongoni mwa watu ambao niliokolewa baada ya kushombwa na maji yam to huo wakati nikivuka kwa ajili ya kwenda kwenye biashara yangu mjini Bariadi lakini namshukuru Mungu niliokolewa,”amesema.



Pendo Magembe ambaye ni mkazi wa Ngashanda amesema kuwa mto  Ngashanda una tabia ya kujaa kipindi cha masika na hakuna mtu anayeweza kuvuka.



“Tuliokuwa tunapata shida ni sisi wananchi wa Ngashanda mto huu ulikuwa ukijaa huwezi kwenda upande wa pili ambapo ndipo kuna huduma zote za msingi za jamii kama vile huduma za afya,mimi nilikuwa mjamzito ulifika muda wa kujifungua nilipofika hapa mtoni nilikuta umejaa maji nikashindwa kuvuka lakini nilipata msaada kutoka vijana ambao waliweza kunivusha na kuniwahisha katika kituo cha afya Muungano mjini Bariadi,”amesema.



Naye Benedictori Ngusa mkazi wa Ngashanda amesema kuwa kuna watu ambao wamepoteza maisha kipindi cha siku za nyuma walipojaribu kuvuka mto huo ukiwa umejaa maji.



“Huu mto ukijaa usilazimishe kupita siku za nyuma wakati daraja hili halijajengwa kuna wenzetu wamekufa hapa kwa kusombwa na maji hasa pale walipokuwa wakilazimisha kuvuka upande wa pili wakati maji yakiwa yamejaa hivyo tunaishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja hili,”amesema.



Mwalimu, Misango Suleiman wa shule ya msingi Ngashanda amesema kuwa faraja kubwa kwao kwa wanafunzi hawatakosa tena masomo kama ilivyokuwa hapo awali pindi mvua inaponyesha.



“Wakati wa kipindi cha mvua,mvua ikinyesha watoto wetu na hata sisi walimu  tulikuwa tunashindwa kwenda shule,tulikuwa tunashindwa kuvuka mto upande wa pili maana ni mpana sana na una maji mengi sana yanakwenda kwa kasi na ikinyesha mfululizo hata siku tatu hakuna kwenda shule hadi maji yapungue,”amesema.



Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Bariadi, Mhandisi Hussein Katakweba amesema kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha usafiri wa wananchi wa maeneo hayo pamoja na mizigo hivyo wananchi watafanya shughuli zao kwa kipindi cha mwaka mzima bila kikwazo chochote kama ilivyokuwa awali,”amesema.



Mhandisi Katakweba amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo Januari 17, 2022 na kukamilika Juni 25, 2025 kwa kuwatumia wakandarasi wazawa ambao ni kampuni ya AUDASIA INVESTMENT COMPANY LTD ya Dar Es Salaam,ITEGAMATU COMPANY LTD ya Shinyanga na SABU ENTERPRISES COMPANY LTD ya Shinyanga.


Kiongozi wa mbio za mwenge, Ismail Ussi  amesema kuwa ameridhishwa na mradi huo na kwamba wananchi watapata huduma nzuri kwa kuwa changamoto iliyokuwepo serikali imeitatua..



Amesema azma ya serikali ni kuona wananchi wake wanapatiwa huduma muhimu katika jamii ili waweze kufanya shughuli zao kwa ajili ya kujipatia kipato.



“Mkuu wa wilaya nikupongeze sana pamoja na Tarura kwa kazi kubwa hii ya ujenzi wa daraja iliyofanyika kwani kama mlivyoeleza wananchi walikuwa wakipata changamoto kubwa sana ya kuvuka upande mmoja kwenda upande mwingine hasa nyakati za mvua za masika,”amesema.



MWISHO. 



Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini(T (TARURA) wilaya ya Bariadi, Mhandisi Hussein Katakweba akisoma taarifa ya ujenzi wa daraja la Ngashanda mjini Bariadi.


Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025,Ismail Ussi akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi katika daraja la mto Ngashanda mjini Bariadi.


Editha Daud ni mkazi wa Ngashanda mjini Bariadi akieleza adha waliyokuwa wakiipata kabla ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Mto Ngashanda.


Benidictor Ngussa mkazi wa Ngashanda mjini Bariadi akieleza adha waliyokuwa wakiipata kabla ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Mto Ngashanda.




Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post