RC MACHA AHAMASISHA USHIRIKI MWENGE WA UHURU-SIMIYU.


Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha akitoa maelezo juu ya ujio wa mbio za mwenge mkoani humo.


Na Samwel Mwanga, Simiyu.


MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, ametoa wito kwa Wazee, Viongozi wa Dini na Vyama vya Siasa mkoani humo kuhakikisha wanahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu kwenye Mbio za Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika kuanzia Agosti 9 hadi 15, 2025.


Macha ametoa wito huo leo, Agosti 7, 2025, wakati akizungumza na makundi hayo katika kikao maalumu kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Nyaumata, wilayani Bariadi.


Akifafanua amesema Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili mkoani Simiyu mnamo Agosti 9, 2025, na utapokelewa rasmi katika eneo la Njia Panda ya Malampaka, wilayani Maswa.


“Nawaomba sana viongozi wetu wa dini, wazee wetu wenye busara, pamoja na viongozi wa vyama vyote vya siasa mkawe mabalozi wa kuhamasisha wananchi washiriki kwa wingi kwenye Mbio hizi za Mwenge. Huu ni wakati wa kuonyesha mshikamano wetu kama Taifa na kuthamini misingi ya Uhuru wetu,” amesema.


Rc Macha amesema kuwa mwenge huo wa uhuru katika mbio zake ndani ya mkoa huo utapitia miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuikagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uwajibikaji, uzalendo na uwazi katika utekelezaji wa miradi ya serikali.


Katika kikao hicho, viongozi mbalimbali walitoa maoni na mapendekezo kuhusu namna bora ya kuhakikisha ushiriki mpana wa wananchi, hususan vijana, katika shughuli zote za Mwenge wa Uhuru mwaka huu.


MWISHO.


Viongozi wa dini wakimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha juu ya ujio wa Mwenge wa uhuru mkoani humo.








Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post