Na Anita
Balingilaki,Simiyu
Jamii mkoa Simiyu
imetakiwa kuchukua hatua dhidi ya matukio au majanga ambayo yanaweza
kuhatarisha maisha yao, watoto na mali zao.
Miongoni mwa matukio
au majanga ambayo yametajwa yanaweza kuepukika ikiwa jamii itachukia tahadhari
za haraka ni pamoja na ajali za barabarani, majini, moto na migodini.
Hayo yamesemwa leo na
kaimu kamanda mkoa Simiyu jeshi la zimamoto na uokoaji Inspekta Faustin Mtitu ambapo amesema kwa
kipindi cha Januari hadi Disemba 2022 jeshi hilo limekabiliana na matukio ya
moto 21 na hakuna mtu aliyepoteza maisha.
Aidha amesema
wamefanya uokoaji kwenye matukio 25 ambayo yanahusisha ajali za barabarani,
migodi, mashimo ya vyoo, kusombwa na maji ya mvua, mabwawa na mito na
yamesababisha vifo 43.
" Matukio hayo
yamesebabisha vifo watu 43 wanawake 14 na wanaume 29 kwa upande wa majeruhi
walikuwa 114 wanawake 38 na wanaume 76 na matukio yote kwa kipindi hicho
hayakihusisha watoto wadogo" amesema inspekta Mtitu.
Katika kuhakikisha
wananchi wanapata elimu dhidi ya majanga Inspekta Mtitu amesema jeshi hilo kwa
kipindi cha Januari hadi Disemba 2022 limeendelea kufanya jitihada za kuzuia
majanga ya moto na majanga mengine yasitokee kwenye jamii kwa kufanya ukaguzi
wa tahadhari na kinga dhidi ya majanga ya moto kwenye majengo na vyombo vya
usafiri na usafirishaji.
" Kwa kipindi cha
mwaka mmoja uliopita ( 2022) majengo 1,537 na magari 76 yalikaguliwa, maeneo 88
yalipatiwa elimu na wanufaika walikuwa 24,754 wakiwemo wanafunzi wa shule za
msingi kuanzia awali, na elimu hiyo waliipata kupitia njia ya redio,
kwenye mashule, nyumba za ibada na kwenye mikusanyiko" amesema
Inspekta Mtitu na kuongeza kuwa:
"Michoro ya
majengo 26 ilisomwa na kupitishwa ikiwemo ya nyumba 17 za kuishi, 05 za
biashara na vituo vinne vya mafuta,...kwa mwaka uliopita hatukupata matukio
yaliyohusisha watoto wadogo ila mwaka 2020 tarehe 19,Novemba watoto watatu
walipoteza maisha kwa kuzama kisimani kwa nyakati tofauti katika kijiji
cha Iwelimo kata ya Mwamanenge wilayani Maswa mkoani hapa" amesema
Inspekta Mtitu.
Annastazia Masanja ni
mkazi wa Kidinda Bariadi amesema jeshi la zimamoto limewasaidia kupata elimu
mbalimbali ikiwemo ya usalama barabrani na elimu hiyo wameifikisha hadi kwa
watoto wao kwa kuwaelekeza namna bora ya kuvuka barabara waendapo shule na
wakati wakirudi.
“Kiukweli mimi elimu
niliyoipata kutoka jeshi la zimamoto na uokoaji…nakumbuka siku moja
nikiwa mnadani walifika wakatupa elimu kwa sasa mwanangu mdogo ana miaka
saba anajua namna bora ya kuvuka barabara kwa kuzingatia alama zilizopo
barabarani” amesema Masanja.
Jisabu Masunga ni
mkazi wa mjini Bariadi amesema ni vema sheria ikachukua mkondo wake ili
kupunguza / kumaliza majanga hususani ambayo yanaepukika huku Veronika Mwobagulalila
akisema bado elimu inatakiwa kwani wapo wanaofanya hivyo pasipo kujua madhara.
" Hivi mtu
anachimba shimo alafu analiacha hivyo hivyo bila kulifukia unakuta jirani na
eneo hilo kuna watoto wadogo sana wengine hata miaka mitano hawajafikia
wanacheza karibu na eneo hilo mtu kama huyo bila sheria kuchukua mkondo wake
makubwa yanaweza kutokea" amesema Masunga.
Miongoni mwa matukio
yaliyoteka hisia za wananchi ni pamoja na ajali za magari ikiwemo ya
iliyotokea Januari 11,2022 iliyotokea eneo la Nyamikoma wilayani Busega mkoani
hapa iliyosababisha vifo vya watu 15, ajali nyingine iliyotokea Marchi 27,2022
iliyotokea Kidurya wilayani Bariadi iliyohusisha vifo vya watu 7 na tukio la watoto
watatu kuzama kwenye visima Novemba 19,2020 wilayani Maswa.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment