MINZA MAYENGA; MAMA ALIYEKATWA MAPANGA NA MUMEWE KISA NG’OMBE NA MASHAMBA

 


Minza Mayenga (47) mkazi wa Mkoa wa Simiyu ambaye ni mama wa watoto tisa aliyekatwa mapanga na mme wake sehemu za kichwa na mkono Novemba 30,2022 akiwa katika hospitali ya wilaya mji wa Bariadi Somanda.

Na Mwamvita Issa 

Kwa siku za hivi karibuni wanandoa wamekuwa ni wahanga wakubwa wa vitendo vya ukatili kwa vazi wanaloliita uvumilivu ili kulinda heshima ya ndoa katika jamii.


Pamoja na mikakati mbalimbali iliyowekwa na serikali ili kukabiliana na vitendo vya ukatili, bado wanawake wamekuwa na mwitikio mdogo katika kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa ikilinganishwa na taarifa zinazotolewa juu ya wanawake na watoto.


Imekuwa ni nadra kwa wanawake kutoa taarifa za vitendo vya ukatili ambavyo wamekuwa wakifanyiwa kwa kujali kulinda mahusiano na kuogopa mtazamo hasi wa jamii baada ya kutoa taarifa hizo.


Katika taarifa ya haki za binadamu kwa mwaka 2021 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mwezi Mei mwaka 2022 ilionesha matukio ya ukatili dhidi ya wanawake yalifikia 23, 685 kwa mwezi, ambapo mikoa inayotajwa kuongoza ni pamoja na Arusha, Manyara, Lindi, Tanga na Mkoa wa Kipolisi Temeke.


Baadhi ya sababu zinazochochea kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake zimetajwa kuwa ni pamoja na kuendelea kushikiliwa kwa mila na desturi zilizopitwa na wakati,elimu duni na mfumo dume wanawake kutomiliki mali katika familia.


Licha ya serikali na wadau wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kutoa elimu hadi vijijini lakini hali bado vitendo hivyo vinaendelea kutokea,kama anavyosimulia Minza Mayenga (47) mkazi wa Mkoa wa Simiyu ambaye ni mama wa watoto tisa aliyekatwa mapanga na mme wake sehemu za kichwa na mkono Novemba 30,2022.


Anasema tukio hilo lilitokea siku mbili baada ya amri ya mwisho ya mahakama juu ya shauri la ndoa namba 112/2022 lilitotolewa na mahakama ya Mwanzo ya Bariadi kituo cha Mhango mkoani Simiyu ikiamuru kupewa stahiki alizokuwa anadai kwa mumewe ili kujikimu pamoja na wanae.


Alikuwa akidai ng’ombe wanne kati ya 11 waliopatikana baada ya kuozesha binti yao pamoja na ekari 8 kati ya 20 walizokuwa wanamiliki.


Minza anasimulia chanzo cha ugomvi kuwa ni baada ya binti yake mkubwa kumjengea nyumba ya kuishi kipindi ambacho mme wake alimuacha na kwenda kuoa mwanamke mwingine.


Anasimulia kuwa, ugumu wa maisha na kukosa matunzo vilimfanya kuhamia kijiji cha Katoryo Kata ya Tegeruka wilaya ya Musoma Mkoani Mara ili kukabiliana na umasikini aliokuwa nao alipokuwa akiishi kijiji cha Ngulyati walayani Bariadi mkoa wa Simiyu.


“Tulivyohamia huko alifika na kunitelekeza nikaanza kuishi nikisaidiwa na kaka zangu hadi binti yangu mkubwa alipokuja na kunijengea nyumba, baada ya miaka mitatu alirudi na alipokuta ile nyumba ugomvi ukaanzia hapo,”anasimulia akiwa na maumivu makali.


“Alikuwa hataki niishi kwenye ile nyumba alikuwa ananipiga na kunitishia kunichoma kisu, baada ya mateso kuzidi ilibidi nihame mimi na watoto tukajenga kijumba kidogo pembeni ya makazi ya kaka yangu na yeye akabaki nyumba kubwa”,anaeleza.


Baada ya muda kidogo kupita mume wake aliuza nyumba ile pamoja na magunia 60 ya mpunga ambayo Minza alilima kwa ajili ya chakula wakati ambao mme wake hakuwepo.


“Maisha yalikuwa magumu sina makazi sina chakula na ninawatoto ilibidi nisafiri hadi Ngulyati kwenda kumuomba anipe ng’ombe wawili wa kulimia na ekari 4 za shamba nipate sehemu ya kulima”,anaeleza.


Anasema mume wake alikataa kumpa kitu chochote ndipo alipofungua kesi katika mahakama ya Mwanzo,kesi ambayo alishinda na hukumu ikatolewa kuwa apewe alichokuwa anakihitaji.


“Baada ya hukumu hakunipa chochote nikawa bado nipo Ngulyati kwa dada yangu ndipo siku moja jioni alinivizia na kunikata mapanga,ninadhani lengo lake lilikuwa ni kuniua kwa sababu nilipoteza fahamu lakini bado aliendelea kunikata hadi watu walipomkamata”,anasimulia Minza.


Minza yupo katika hospitali ya wilaya mji wa Bariadi Somanda, akiendelea kupatiwa matibabu huku sura yake ikiwa imeshonwa na nyuzi nyingi ambazo ni ngumu kuzihesabu, mme wake Buluba Nkalango anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Simiyu.


Wakati vitendo vya ukatili wa kijinsia vinazidi kuongezeka nchini Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, Januari 22, 2022 akiwa katika hafla ya uzinduzi wa dawati la jinsia katika Taasisi za elimu ya juu na Kati,Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alitaja jitihada sita ambazo Wizara yake imeanzisha ili kupambana na hali hiyo.



Anasema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA),ambapo jitihada hizo zimewezesha kuongezeka kwa idadi ya watu wanaotoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia kwa vyombo husika na kwa kipindi cha mwaka 2020/21 jumla ya matukio 20,025 ya ukatili yaliripotiwa ikilinganishwa na matukio 18,270 yaliyoripotiwa kwa mwaka 2019/20.


Waziri Gwajima alisema baadhi ya wanawake wameendelea kuwa waathirika wa vitendo vya ukatili kwa kuendelea kuamini kuwa ni wajibu wao kuendelea kuwa katika ndoa hata kama wanakumbana na mateso na manyanyaso pia kuogopa maneno ya watu katika jamii pale wanapoondoka kwenye ndoa.


Emmanuel Martine ni mdau wa kupinga ukatili kwa wanawake na watoto kutoka katika shirika lisilo la kiserikali la World Vision linaendesha mradi wa maendeleo katika wilaya ya Itilima mkoani Simiyu anasema imekuwa ni kichaka cha wanaume kuwatendea maovu kwa sababu katika jamii hiyo inaamini mwanamke anayeachika kwenye ndoa anakuwa hana maadili.


“Kuna haja ya wadau kutafuta namna na njia mbalimbali za kuwaelimisha wanawake pamoja na wanamme ambao wamekuwa wakifanya ukatili huo ili kila mmoja awe ni mlinzi wa mwenzake”,anasema.


Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Ushirika wa Tumaini Bariadi Prosper Shayo anasema ni wajibu wa jamii kuangalia ni vitu gani vinapunguza upendo baina yao hali inayochochea migogoro na ukatili uliopitiliza.


“Ningeomba jamii kujifunza mambo matatu ambayo ni upendo uvumilivu na uaminifu, tuwafundishe upendo ili kila mmoja akipenda mwenzake hatutaona ukatili huu unaoendelea,” anasema mchungaji Shayo.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم