Tarura maswa kutumia Bilioni 4 kutengeneza, kukarabati Barabara.


Kaimu Meneja wa Tarura wilaya ya Maswa,Mhandisi Francis Kuya akiwakilisha bajeti ya Tarura Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 katika baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
 


Baadhi wa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa wakiwa katika Kikao Cha Bajeti Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo bajeti ya Tarura iliwasilishwa.

Na Samwel Mwanga,Maswa.

 

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini(TARURA)katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu  katika mwaka wa fedha 2023/2024 imekadiria  kutumia kiasi cha Sh. Bilioni 4,226,273,478.26 kwa ajili kukarabati, kufanyia matengenezo na kujenga mtandao wa Barabara Wilayani humo.

 

Kaimu Meneja wa TARURA wilayani humo Mhandisi  Francis Kuya akiwakilisha bajeti hiyo kwenye Kikao Cha Baraza la Madiwani amesema kuwa  bajeti hiyo imezingatia vipaumbele ambavyo ni pamoja na hali ya barabara,barabara zinazopita maeneo ya uzalishaji.

 

Vipaumbee vingine ni kuendeleza maeneo ya miji yenye idadi kubwa ya watu,barabara ambazo serikali umeweka miundombiniu mikubwa na vipaumbele vya barabara katika kila Kata 

 

Akielezea mchanganuo wa utekelezaji wa bajeti hiyo Mhandisi Kuya amesema kuwa Sh Bilioni 1.2 ni kutoka mfuko wa barabara kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa Km 141.21,Ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua  mita 800 na madaraja matatu.

 

Ameendelea kueleza Sh Bilioni Moja kutoka mfuko wa Jimbo kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami Maswa mjini kilomita moja,Ujenzi wa madaraja mawili,Ufunguzi na Ukarabati wa Barabara Kwa kiwango cha changarawe Km 21.45

 

Pia Mhandisi Kuya amesema kuwa Sh bilioni 2 kutokana na tozo za mafuta kwa ajili ya Ufunguzi na Ukarabati wa Barabara km 92 na uwekaji wa taa za barabarani Maswa mjini na Sh Milioni 216.2 ni fedha za utawala na Usimamizi wa miradi.

 

"Tumeziangalia pia barabara za Vijijini katika bajeti hii na Kwa miradi ya matengenezo ya kawaida Kuna barabara ya Isagenghe-Zabaza-Nyashimba,Masanwa-Buhungukila na Mwasayi-Masela-Wigelekelo,"

 

"Barabara nyingine ni pamoja na Bugarama-Mwabomba-Mwanundi,Isageng,he -Budekwa-Mwabaraturu na Njiapanda-Muhida-Jihu,"amesema.

 

Mhandisi Kuya amesema kuwa Matengenezo ya maeneo korofi,Matengenezo ya muda Maalum na Ujenzi wa madaraja na Mitaro nayo yameguswa katika maeneo mbalimbali ya vijijini.

 

Amesema kuwa fedha zinazotokana na tozo za mafuta zitafanya ukarabati wa barabara  urefu wa Km 47.00 Kwa Jimbo la Maswa Mashariki na barabara zenye urefu wa Km 45.00 katika Jimbo la Maswa Magharibi.

 

 Baadhi ya madiwani wakichangia bajeti hiyo walisema kuwa ni nzuri Kwa kuwa imegusa maeneo mengi ya vijijini ambalo ndiko kuna changamoto kubwa ya miundombiniu ya barabara.

 

"Ukiiangalia hii bajeti kwa kweli ni nzuri kwa sababu imegusa maeneo mengi ya vijijini ambalo huko ndiko kuna changamoto ya barabara na nyingi zinakuwa mbovu hivyo Kwa Tarura kuwekwa nguvu huko ni kuonyesha walivyojipanga kuwahudumia wananchi wa Wilaya ya Maswa,"amesema Jeremiah Shigala diwani wa Kata ya Zanzui.

 

Tarura katika wilaya ya Maswa inahudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya Km 1084.2 ambapo barabara za changarawe ni Km 581.15,barabara za udongo ni Km 499.27 na barabara za lami ni Km 3.78

 

MWISHO.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post