Makala| Njalu Silanga: Miaka 20 wananchi waliteseka, tumefanya mageuzi makubwa miaka 7.

Mbunge wa Jimbo la Itilima Mkoani Simiyu Njalu Silanga akizungumza na wananchi wa Jimbo lake la Itilima, wakati wa sherehe za miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika kiwilaya katika kijiji cha Ndoleleji.

Mbunge wa Jimbo la Itilima Mkoani Simiyu Njalu Silanga akizungumza na wananchi wa Jimbo lake la Itilima, wakati wa sherehe za miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika kiwilaya katika kijiji cha Ndoleleji.

 



Mbunge wa Jimbo la Itilima Mkoani Simiyu (kulia) akisalimia na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Yahya Nawanda (mwenye miwani) mara baada ya viongozi hao kuwasili kwenye sherehe za miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika kiwilaya katika kijiji cha Ndoleleji.

Na Derick Milton, Itilima.

 

“ Nilianza harakati za siasa mwaka 2007 baada ya vijana wa Mkoa wa Simiyu kuniamini kwa kunipigia kura 664, kati ya kura 668, vijana wanne tu ndiyo walisema sitoshi kuwa mjumbe wa Mkutano mkuu CCM”

 

Ni maneno yake Mbunge wa Jimbo la Itilima Mkoani Simiyu, Njalu Daudi Silanga (CCM), anatajwa kuwa mbunge namba moja ndani ya mkoa huo anayeungwa mkono zaidi na wananchi wote wa jimbo lake hata wale kutoka vyama shindani.

 

Hadi anafikia hatua ya kuwa mwakilishi wa wananchi wa jimbo hilo kwenye chombo cha kutunga sheria (bunge), Njalu anasema haikuwa kazi rahisi kupambana na vigogo wa siasa kutoka vyama shindani.

 

Kutoka mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM (MNEC) na Mbunge wa Jimbo la Itilima, alisukumwa zaidi na mateso ya wananchi wa jimbo hilo waliyoyapata kwa miaka 20.

 

Chini ya vigogo wa siasa John Cheyo (UDP), Dany Makanga (UDP) na wengine wengi wakiwemo Edward Ng’wani, zaidi ya miaka 20 wananchi waliteseka na miundombinu mibovu ya Barabara.

 

Ukosefu wa huduma za Afya ilikuwa changamoto nyingine iliyowatesa, ukosefu wa maji safi na salama, kutokuwepo kwa mazingira rafiki ya upatikanaji wa elimu iliyo bora kwa wananchi wa Jimbo hilo.

 

Utekelezaji wa Ilani.

 

Wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa wananchi wa Jimbo hilo jana, wakati wa sherehe za miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika katika kijiji cha Nangale kata ya Ndoleleji.

 

Anasema baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 2015, kazi yake ya kwanza ilikuwa kuhakikisha anatatua changamoto ya miundombinu ya Barabara ambayo ndiyo ilikuwa kilio kikubwa cha wananchi.

 

“ Nikiwa na Madiwani 7 kutoka CCM kati ya 22, tulifanya kazi kubwa usiku na mchana ya kuhakikisha jimbo la Itilima linabadilika, wananchi wanaanza kuonja raha ya maendeleo na kupata huduma bora za kijamii,” anasema Njalu.

 

Miundombinu ya Barabara.

 

Mbunge huyo anasema kuwa kwa kipindi cha miaka saba, Wilaya ya Itilima imefunguka, kila sehemu panapitika kwa nyakati zote tofauti na ilivyokuwa awali ambapo hakuna gari ilifika kijijini.

 

Anaeleza kuwa Wilaya hiyo inazo Barabara kubwa na muhimu zipatazo 82, ambapo kwa sasa Barabara zote zimefunguliwa na zinapitika muda wote na wananchi wanafanya shughuli zao kwa furaha.

 

“ Kila mwaka nimekuwa nikihakikisha tunatapa fedha za kutengeneza Barabara zetu, kwa sasa unaweza kuingia na kutoka Wilaya ya Itilima kwa kupitia sehemu yeyote, hakuna kikwazo hata kimoja”…..

 

“ Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suruhu Hassan kwa kuendelea kutuletea fedha nyingi kwenye eneo la Barabara, na katika bajeti ya mwaka huu ametupatia kiasi cha Sh. Bilioni 2.7 kwa ajili ya Barabara tu,” anasema Njalu.

 

Huduma za Afya.

 

Njalu anasema kuwa wakati anaomba kura kwa wananchi kipaumbele chake cha pili ambacho aliwahidi wananchi, ni kuhakikisha wanapata huduma bora za Afya na kwa karibu.

 

Anasema jambo la kwanza kulifanyia kazi baada ya kuchaguliwa, lilikuwa kuhakikisha Wilaya hiyo inapata Hospitali ya Wilaya, jambo ambalo alilifanikisha kwa kiwango kikubwa na Wilaya ina Hospitali ya Wilaya.

 

“ Wananchi sasa hawafuati huduma Wilayani Bariadi, Hospitali yetu inafanya kazi na inatoa huduma zote, Rais Dkt. Samia ametulileta Milioni 500 kwa ajili ya kuboresha Hospitali yetu na tunaendelea na maboresho”

 

Anasema kuwa kwa kipindi cha Mwaka mmoja wa Rais Dkt. Samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati 8 pamoja na ujenzi wa kituo kingine kimoja cha Afya cha Mwanunda na kimekamilika.

 

Elimu.

 

Anasema kuwa Wilaya hiyo ilikuwa nyuma kielimu kutokana na mazingira, huku mwitikio wa wananchi kupeleka watoto shule ukiwa chini, ambapo kwa kushirikiana na wananchi wameweza kujenga shule mpya 16.

 

“ Katika Elimu tunaishukuru serikali imeendelea kuboresha mazingira, tumepokea zaidi ya Bilioni 3 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya wanafunzi na walimu kwa kujenga madarasa na nyumba za walimu,” anaeleza Silanga.

 

Huduma ya maji.

 

Chagamoto kubwa nyingine ambayo wananchi wa jimbo hilo wameteseka nayo kwa muda mrefu ni upatikanaji wa maji safi na salama, ambapo awali walipata maji kwenye madimbwi na mabwawa ya kuchimba wenyewe.

 

Mbunge huyo akizungumzia suala la huduma ya maji, anaeleza kuwa kwa kiwango kikubwa huduma hiyo imeboreshwa, na wananchi maeneo mengi wameanza kuonja maji safi na salama.

 

“ Pale makao makuu yetu ya Wilaya Lagangabilili, walikuwa hawajawahi kupata maji safi na salama, lakini nilipoingia nilihakikisha tunapata mradi mkubwa wa maji, na sasa wanapata maji kila siku … maji safi na salama”

 

“ Katika kijiji hiki cha Ndoleleji serikali imeleta kiasi cha zaidi ya Sh. Milioni 192 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu cha maji, muda siyo mrefu tutapata maji safi na salama hapa”

 

Anaeeleza kuwa mbali na hilo, kuna mradi mkubwa wa kutoa maji ziwa Victoria, ambapo Jimbo lake limewekwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo, hivyo wananchi watarajie kupata maji kutoka ziwa Victoria.

 

Huduma ya Umeme.

 

Njalu anasema kuwa hadi kufikia Mwezi Aprili mwaka huu, vijiji vyote 102 katika jimbo hilo vitakuwa na umeme, ambapo baada ya hapo wataanza kupeleka umeme kwenye vitongoji.

 

“ Serikali ya Mama Samia, tayari imetutengea kiasi cha Sh. Bilioni 14 kwa ajili ya kusambaza umeme, ambapo Mkandarasi Sengerema Company Ltd anaendelea na zoezi la kupeleka umeme katika vijiji vyote” anasema Njalu.

 

Michezo.

 

Mbunge huyo anasema kuwa suala la michezo halijaachwa nyuma, kwani tangu amechaguliwa alianzisha mashindano ya Njalu Cup, mashindano ya mpira wa miguu ambayo yamekuwa maarufu na kuleta furaha, amani na upendo baina ya wananchi wa jimbo hilo.

 

Hata hivyo Mbunge huyo anasema kuwa kazi bado haijamalizika katika jimbo hilo, kwani baadhi ya maeneo bado yameendelea kuwa na changamoto, ambapo yeye na viongozi wa Wilaya wakiwemo madiwani wataendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa.

 

Anasema kuwa kuendelea kuwa Mbunge kwenye jimbo hilo, atahakikisha anawatumikia wananchi wa jimbo hilo kwa nguvu zote, ikiwa pamoja kuhakikisha anashirikiana nao katika kuleta maendeleo.

 

“ Kazi bado haijaisha, tuliteseka sana miaka 20, lakini sasa tuna miaka 7 tumeanza kuonja matunda, kazi bado haijamalizika, mimi pamoja na viongozi wengine na madiwani, tumesema lazima tuwatumikie”

 

Njalu anawataka wananchi hao kutoa ushirikiano kwa serikali na wadau wa maendeleo, ikiwemo kupeleka watoto shule kwani kazi kubwa imefanyika ya kuboresha elimu mashuleni.

 

“ Kwenye Wilaya hii, chini yangu, chini yangu, na kwa umri wangu huu, hakuna mwananchi atateseka kama ambavyo mliteseka miaka 20 nyuma, tumejipanga kuhakikisha tunawahudumia,” amesema Njalu.

 

MWISHO.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم