CCM yampongeza Rais Samia Utekelezaji wa Miradi Bariadi.



MKUU wa Wilaya ya Bariadi Mkoa wa Simiyu Saimon Simalenga akiwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2022/2023 kwenye ukumbi wa CCM mjini Bariadi.


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bariadi Juliana Mahongo akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya hiyo wakati wakimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwa kwenye mkutano.

 

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu Tinana Masanja akiongea kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu uliofanyika ukumbi wa CCM mjini Bariadi.

 

Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo katika sekta za Afya, Elimu, Maji, Umeme, Barabara na Miundombinu.

 

Aidha Chama hicho kimesema kitahakikisha Rais Samia anashinda katika uchaguzi ujao (2025) ili aweze kukamilisha utekelezaji wa miradi inayoendelea ambayo imeleta tija na kuwaondolea adha wananchi ikiwemo miradi ya maji na barabara.

 

Hayo yamebainishwa leo na Mwenyekiti wa Chama hicho, Juliana Mahongo mara baada kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2022/2023 iliyowasilishwa kwenye mkutano uliofanyika ukumbi wa CCM mjini Bariadi.

 

Juliana amesema CCM wilaya ya Bariadi imemwondolea wasiwasi Rais Samia, na kumtaka kuendelea kuchapa kazi na hivyo inamwomba afanye ziara ya kikazi wilayani humo ili waweze kumpongeza ana kwa ana.

 

‘’Rais Samia ameiheshimisha Tanzania, Afrika na Dunia kwa Ujumla…anaendelea kutekeleza miradi mikubwa ambayo itakwenda kuwa kutovu cha uchumi wa nchi yetu, amendelea kutekeleza miradi ya maji, afya, elimu, barabara, umeme na ujenzi wa miundombuni katika sekta za elimu na afya’’ amesema Mwenyekiti huyo.

 

Amewataka Madiwani na viongozi wengine kutangaza mazuri yanayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita ambapo kila kijiji, mtaa na kata kuna miradi ya maendeleo inatekelezwa.

 

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wilaya ya Bariadi (UVCCM) Tinana Masanja amewahimiza Madiwani, wenezi wa kata kusimama imara katika kutangaza utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

 

Alisema ndani ya miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan, kila kijiji, kata au mtaa kuna mradi wa maji au barabara unaotekelezwa na serikali ya awamu ya sita, hivyo viongozi wa Chama ngazi ya kata na matawi hawana budi kuitangaza.

 

Naye Leah Mahuma, Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Gamboshi aliipongeza serikali ya Rais Samia kwa kuwatua akina mama ndoo kichwani katika kata hiyo ambao walikuwa wakihangaika usiku na mchana kusaka huduma ya maji.

MWISHO.

 

Wajumbe wakiwa kwenye mkutano.


Wajumbe wakishangilia kwenye Mkutano.
 
 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post