Na COSTANTINE MATHIAS, Itilima.
SERIKALI kupitia Bodi ya Pamba nchini (TCB) imenunua ndege 20 zisizokuwa na rubani kwa ajili ya kunyunyizia dawa za kuuwa wadudu kwenye zao la pamba.
Aidha, kati ya ndege hizo, ndege saba zimepelekwa mkoani Simiyu kwa ajili ya kunyunyizia mashamba makubwa ya pamba na kwamba mkulima atanyunyiziwa shamba lake bila gharama yoyote.
Akizungumza na Waandishi wa habari wakati wa majaribio ya ndege hizo, Mhandisi kutoka Bodi ya Pamba Kisinza Ndimu alisema wamefanya majaribio katika wilaya ya Itilima kwa kutumia ndege zisizo na rubani ambazo zitatumika kupulizia mashamba makubwa ya Pamba.
Amesema Bodi ya Pamba imekuwa ikitoa pembejeo kwa wakulima wake, ikiwemo mbegu, viuatilifu pamoja ni Pampu za kupulizia ambazo hubebwa mgongoni.
‘’kwa hali ilivyo kwa sasa na sababu wakulima wengi wana mashamba makubwa, tumeona ili kurahisisha kazi tuwaletee ndege zisizo na rubani (drone)…Bodi Pamba kupitia serikali tumenunua drone 20 na zimepelekwa kwa wakulima wilayani kwenye mashamba makubwa’’ amesema.
Amesema kuwa mashine hizo zitasaidia wakulima wa pamba kutumia muda mchache wakati wa kupulizia, kwani pampu za kawaida (matabi) mkulima alikuwa anatumia muda mwingi kupulizia na kuchoka hasa akiwa na shamba kubwa.
Ameongeza kuwa mashine hizo zina uwezo wa kupulizia ekari 15 mpaka 20 kwa saa 1 jambo ambalo litampunguzia adha mkulima ya kupiga shamba kubwa kwa muda mrefu.
Kisinza amewataka kuzitunza mashine hizo ili ziweze kudumu na kutumika kadri serikali ilivyokusudia na kwamba matumizi ya ndege hizo yataongeza uzalishaji wa zao la pamba.
Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Itilima Said Itaso amesema amepokea mashine ya kupulizia wadudu wa pamba shambani ili kuweza kuwasaidia wakulima wenye mashamba makubwa ambao walikuwa wanatumia muda mwingi kupulizia kwa kubebea pampu mgongoni.
Amesema awali walikuwa wanakutana na changamoto ya upuliziaji kwa wakulima wakubwa wa pamba ambao walikuwa wanahitaji teknolojia ili kurahisisha zoezi la upuliziaji wa mashamba yao.
‘’changamoto kubwa nilikuwa naipata kwa wakulima wenye mashamba makubwa kuanzia eakri 10, 20 mpaka 50…walikuwa wakitumia watu wengi kupulizia shamba kubwa kwa siku nyingi, lakini mashine hii imekujwa kwa muda mwafaka kuwasaidia, niko tayari kuwasaidia wakulima wenye mashamba makubwa’’ amesema Itaso.
Kwa upande wao wakulima wa Pamba kutoka kijiji cha Budalabujiga wameipongeza serikali kupitia Bodi ya Pamba kwa kubuni ndege zisizokuwa na rubani kwa ajili kusaidia wakulima wenye mashamba makubwa.
Salu Omela mkazi wa Budalabujiga, amesema wakulima wengi walishindwa kulima mashamba makubwa kutokana na changamoto wakati wa kuupulizia wadudu shambani.
Naye Sayi Mahunga mkulima wa Kijiji cha Budalabujiga amesema teknolojia nya ndege isiyo na rubani itawasaidia wakulima kupulizia eneo kubwa kwa muda mfupi.
Amesema kupitia teknolojia hiyo wadudu watafikiwa kirahisi na dawa kutokana na msukumo (pressure) wa mashine na pia wakulima wataongeza uzalishaji wa zao la pamba.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment