Na Derick Milton, Bariadi.
Ombi la Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa
Mazingira Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu (BARUWASA) kutaka kuongeza bei za maji kwa watumiaji wadogo
na wakubwa limekubaliwa na wananchi huku huduma zikitakiwa kuboreshwa.
Mamlaka hiyo kupitia bodi yake, ilipendekeza bei mpya za maji
na kupeleka maombi yake kwenye Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji
(EWURA) kwa ajili ya kupitiwa.
Kama ilivyo utaratibu maombi hayo lazima yajadiliwe na
watumiaji wa huduma hiyo (wananchi) kabla ya kupitishwa, ambapo Jana Ewura waliendesha mkutano wa
wananchi ambao ndiyo watumiaji wa huduma hiyo katika mji wa Bariadi.
Kabla ya majadilino Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Musalila Masatu alisoma mapendekezo ya bei mpya ambazo zinaombwa kuongezeka, ikiwa pamoja na kueleza sababu za hatua hizo.
Masatu alisema kuwa bei ambazo zinatumika kwa sasa, zilianza
kutumika toka mwaka 2014 ambapo baadhi ya gharama za vifaa zilikuwa chini
lakini kwa sasa gharama zimependa ikiwemo na kuongezeka kwa gharama za
uendeshaji wa mamlaka hiyo.
Amesema kuwa kwa bei za sasa wateja wa majumbani Unit moja
sawa na lita 1,000 au ndoo za maji 50 bei yake ni sh. 660, wateja wa taasisi ni
Sh. 780, wateja wa Biashara ni sh.900 na wateja wa vioski ni Sh. 1,000.
“ Kwa bei hizi ni sawa ndoo moja kwa wateja wa majumbani tulikuwa
tunatoza Sh.13.20, Taasisi Sh.15.60, Biashara Sh.18 na vioski Sh.20.
Bei Mpya zinazoobwa.
Mkurugenzi huyo wa BARUWASA amewasilisha bei mpya zinazoombwa
na Mamlaka hiyo kuwa ni:-
Kwa wateja wa ndani
kutoka Sh.660 kwa Unit moja hadi Sh.1,133 sawa na Sh. 22.66 kwa ndoo moja, kwa
wateja wa taasisi kutoka Sh.780 hadi Sh.1,405 sawa na ndoo moja Sh.28.10,
wateja wa Biashara kutoka Sh.900 hadi Sh.1,513 sawa na ndoo moja Sh.30.26.
“ Tumeongeza pia na bei za viwanda maana uko nyuma hatukuwa
na viwanda, sasa tumeomba bei iwe Sh.2,093 sawa na ndoo moja Sh.41.86, Lakini
pia Vioski kutoka Sh.1,000 hadi Sh.1,790 sawa 35.80”
Mkurugenzi huyo alisema kuwa kuongezwa kwa bei hizo kuna
baadhi ya vifaa vimeongezeka bei, kama mabomba ya kusambazia maji, pamoja na
vifaa vingine, gharama za uendeshaji, lakini pia hitaji la wafanyakazi kwa
ajili ya kuongeza ufanisi wa mamlaka”
Baada ya Mkurugenzi kuwasilisha bei hizo, wananchi waliridhia
na kusema kuwa bei kwao siyo tatizo, ambapo wametaka huduma ziboreshwe zaidi
ikiwemo kuongeza siku za kutoa huduma za maji.
“ Sisi kwetu kwa hizi bei mpya hazina shida, ni bei za
kawaida, tunachotaka sisi ni maji basi, maji yatoke kila siku, siyo leo
tunawapitishia alafu kero zinabaki vile vile,” alisema Sanane Shenye.
Mmoja wa wananchi kutoka mtaa wa Budeka alisema kuwa bei
kwake siyo tatizo, ambapo alieleza tatizo kubwa ni huduma zinazotolewa na
BARUWASA, baadhi ya wateja katika mtaa huo wanaweza kukaa mwezi mzima bila ya
maji.
“ Mimi kwenye mtaa wangu tunataka maji, hatuna shida na bei,
tunataka maji saa 24, akina mama kule kwangu wanateseka, wanakaa mwezi mzima
bila ya maji, sisi tunataka maji,”
Hata hivyo wengi waliridhia bei hizo zitumike, ambapo
walisistiza zaidi kuboreshwa kwa huduma, ikiwemo kuongeza mtandao wa maji,
pamoja na kupewa kipaumbele cha kupata maji wananchi ambako vyanzo vya maji
vinapatikana.
Mkuu wa Mkoa huo Dkt Yahya Nawanda akaitaka Bodi ya BARUWASA,
kuhakikisha ongezeko la bei mpya za maji linakwenda sambamba na uboreshwaji wa
huduma kwa wananchi.
“ Bodi mmesikia maoni ya wananchi, wao hawana shida na bei na
wamepitisha, wanachotaka ni maji, huduma ziboreshwe, na mimi nawaagiza
hakikisha huduma zinaboreshwa na mnatatua kero za wateja wenu,” alisema
Nawanda.
Hata hivyo bei hizo hazitaweza kutumika kwa sasa, mpaka
mchakato wa kufikia hatua ya kutangwa rasmi ukamilike chini ya EWURA.
MWISHO.
Post a Comment