Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Simiyu Ester Midimu ametoa kiasi cha shilingi mil. 12 kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya wanawake vya Umoja wa Wanawake (UWT) wilaya ya Maswa.
Akizungumza juzi mara baada ya kukabidhi fedha hizo amesema anaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita ambayo inatoa mikopo kwa vijana, wanawake na walemavu ili kuwawezesha kiuchumi.
Alisema atahakikisha anawezesha Umoja wa Wanawake Mkoa wa Simiyu ili waweze kujitegemea hali ambayo itawajengea uwezo wa kujiinua na kujikwamua kimaisha.
‘’Nitahakikisha napita wilaya zote za Mkoa wa Simiyu kuwezesha wanawake ili kumuunga mkono Rais Samia kuwakwamua wanawake wenzangu kiuchumi kwa kuwawezesha mitaji’’ alisema.
Katika hatua nyingie, Mbunge Ester aliwataka Umoja wa Wanawake (UWT) mkoani humo kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan juu ya jitihada zake za kuwaletea maendeleo wananchi.
Amewasisitiza pia, kuyasema mazuri yanayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita kwenye miradi ya maendeleo katika sekta za Maji, Afya, Elimu, Umeme na Barabara.
Aliwasisitiza pia kulinda na kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita ili iweze kunufaisha vizazi na vizazi kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Simiyu Mariam Manyangu alimpongeza Mbunge huyo kwa kuwashika mkono na kuwawezesha kiuchumi wanawake hao.
Alisema kuwa mwanamke akijikwamua kiuchumi anao uwezo wa kuendesha familia na kukuza uchumi wa Taifa, lakini pia ana uwezo wa kulinda rasilimali za taifa.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo aliwasisitiza wanawake hao kumuunga mkono Rais Samia ambaye amejikita kuwatua ndoo za maji akina mama katika maeneo yote nchini.
‘’Rais Samia ameendelea kutekeleza miradi ya Maji kwa kila kata au kijiji, miradi ya barabara, umeme, vyumba vya madarasa ya sekondari na msingi…tumuunge mkono Mwanamke mwenzetu anayeendelea kutupigania wanawake’’ alisema Mariam.
Naye Katibu wa UWT, Mkoa wa Simiyu Mondester Mwaya alisema watahakikisha ifikapo 2025 wanampa kura za kishindo Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema Umoja wa Wanawake Mkoa wa Simiyu wamejipanga kuhakikisha hawamwangushi Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mwanamke kinara wa maendeleo nchini.
MWISHO.
Post a Comment