Na Mwandishi Wetu
MJADALA wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) unaoendelea baada ya kuwasilishwa kwake bungeni Dodoma wiki hii, umeacha nje jambo moja – nafasi na umuhimu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye jambo hilo.
Ni rahisi kuelewa kwa nini macho na masikio ya wengi yataelekezwa kwenye taarifa kuhusu kinachoonekana kama matumizi mabaya na upotevu mkubwa wa mali ya umma yaliyomo kwenye ripoti hiyo. Mara nyingi taarifa ya CAG huumiza na kukera wengi.
Wakati akipokea taarifa hiyo ya CAG wiki mbili zilizopita, Rais Samia hakutofautiana na wengi na – kwa kuonyesha namna alivyokerwa na yaliyomo, alitumia lugha kali ambayo Watanzania hawajazoea kumsikia akizungumza hadharani.
Lakini huo ni upande mmoja wa shilingi. Upande wa pili wa shilingi ni kwamba kama Rais Samia angetaka kuficha madudu yaliyomo serikalini kwake, angeweza kufanya hivyo kama ilivyo kwa viongozi wengine wa Kiafrika na duniani wasiopenda dhana ya uwajibikaji ndani ya serikali zao.
Katika dunia ya sasa, desturi kwa viongozi wakubwa wa dunia ni kuingia madarakani kihalali na kuanza kupambana na vyombo na taasisi zinazoweza kubana mamlaka ya watawala au kuibua uozo uliomo serikalini na kwenye maisha ya watawala.
Njia wanazotumia viongozi wengi ni kuviondolea uhalali vyombo na watu waliojitolea kupambana na uozo, kuvipunguzia bajeti ili visitimize majukumu yake na wakati mwingine kuvifuta kabisa.
Mdhibiti Mkuu kwenye Siasa za Tanzania
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni taasisi ambayo iko kikatiba. Hata hivyo, katika miaka walau 40 ya kwanza ya Uhuru, nafasi ya CAG (ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa NAOT), haikuwa na umaarufu wala ushawishi ilionao sasa.CAG wa kwanza Mzalendo, Mohamed Aboud, alidumu kwenye nafasi hiyo kuanzia mwaka 1969 hadi 1996. Alifuatiwa na Thomas Kiama aliyeanza mwaka 1996 hadi alipostaafu mwaka 2005.Ofisi hiyo ilianza kubadilika mwaka 2005 wakati alipoingia Ludovick Utouh.
Ukizungumza na Watanzania wengi, utadhani kwamba Utouh ndiye alikuwa CAG wa kwanza hapa nchini. Hata hivyo, Utouh alikuwa vile alivyokuwa kwa sababu moja tu; Jakaya Kikwete.Rais Kikwete ndiye aliyeibadili ofisi ya NAOT kisheria na kimajukumu kufanya inachofanya sasa.
Aliongeza bajeti kubwa iliyofanya ofisi hiyo kuongeza idadi ya wafanyakazi na utaalamu kiasi kwamba kufikia mwishoni mwa utawala wake, ofisi hiyo ilipewa kazi ya kukagua vitabu vya hesabu vya Umoja wa Mataifa (UN).
Isingewezekana kwa CAG Utouh kufanya yote aliyofanya bila Kikwete.
Kama Rais huyo wa nne wa Tanzania asingetaka, NAOT ingeweza tu kuendelea na shughuli zake kama ilivyozoea au kama ilivyo kwenye nchi nyingi za kiafrika ambako haina meno.
Kama kulikuwa na migogoro yoyote baina ya Utouh na Serikali ya Kikwete hatukuwahi kuisikia.
Tulichokuwa tunasikia ni kuwa bajeti ya CAG ilikuwa inaongezeka kila mwaka na majukumu ya kikaguzi kuongezeka ndani na nje ya nchi.
Alipoingia madarakani hayati Rais John Magufuli, kulikuwa na migongano ya wazi baina yake na Profesa Mussa Assad aliyechukua nafasi ya Utouh baada ya kustaafu kwake.
Miaka mitatu tu baada ya kuingia madarakani, bajeti ya CAG ilikatwa kutoka shilingi bilioni 69.1 mpaka shilingi bilioni 61.4.
Mafunzo zaidi kwa watumishi wa ofisi hiyo yakaanza kuadimika na mawanda ya ukaguzi yakapunguzwa.
Hali ikawa mbaya kiasi kwamba ikafikia wakati Bunge likakataa kufanya kazi naye – pengine kwa maelekezo ya Mkuu wa Nchi na mwishowe Assad akaondolewa kwenye wadhifa huo kinyume cha taratibu.
Kama kuna funzo moja la kudumu kwenye historia ya Tanzania ni kwamba uimara na uhuru wa CAG kwenye kutimiza majukumu yake unaendana moja kwa moja na Rais aliye madarakani. Kama Rais anataka ripoti ya CAG iwe imara na thabiti, ripoti ya CAG itakuwa imara na yenye weledi.
Rais Samia na CAG
Wakati Rais Samia anaingia madarakani mwaka 2021, nchi ilikuwa inapita katika kipindi kigumu kiuchumi kutokana na athari za ugonjwa wa Uviko-19 uliosababisha kuyumba kwa uchumi wa dunia.
Pamoja na hayo, miongoni mwa hatua za awali alizochukua – katika mazingira hayo magumu, ilikuwa ni kuongeza bajeti ya ofisi ya CAG kutoka shilingi bilioni 80 alizokuta hadi bilioni 80.9.
Zaidi ya hapo, tangu siku yake ya kwanza madarakani, Rais amekuwa akitoa ujumbe wa mara kwa mara wa kutaka taasisi za uwajibikaji na zile za utoaji haki kutimiza majukumu yao waliyopewa kikatiba.
Kwa kufanya hivyo, alikuwa anamtia moyo CAG Charles Kicheere, kuwa anachotakiwa kufanya ni kutimiza wajibu wake.
Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha takribani miaka minne iliyopita, CAG aliruhusiwa kufanya ukaguzi katika maeneo kama ya manunuzi ya ndege za serikali ambayo yalikuwa ‘kaa la moto’ kuyajadili wakati wa zama za mtangulizi wake.
Kwa sababu ya kuwepo kwa uhuru wa kutosha wa wanasiasa, wanaharakati, wabunge na waandishi wa habari, ina maana ripoti ya CAG ya safari hii itakuwa na mwangwi mkubwa pengine kuliko ilivyokuwa miaka michache nyuma.
Lakini Watanzania sasa wanajua kwamba haya yote ni matunda ya utawala wa Rais Samia.
Kama angeamua kufuata nyayo za mtangulizi wake, tungesikia na kujadili yale tu ambayo watawala wangetaka tuyasikie na kuyajadili.
Kama tunasikia vitendo vya ubadhirifu na ufisadi, maana yake ni kwamba Rais Samia anataka kujua wapi panapovuja ili hatua zichukuliwe.
Hata hivyo, ni hatari sana kumlazimisha Rais aanze kuchukua hatua tu kwa sababu amekerwa na alichokisoma na kuambiwa.
Ili tusirudi tulikotoka na kumfanya Rais abaki kuvipa nguvu vyombo vyake, ni muhimu mchakato na taratibu za kihasibu na kisheria kufuatwa ili kwamba kama mtu atakutwa na hatia, aadhibiwe baada ya kukamilika kwa mchakato wa uchunguzi.
Wale wote wanaotaka Rais achukue hatua za papo kwa papo sasa hivi bila ya uchunguzi wa makini kwa sababu ya ripoti hii, hawaitakii mema nchi yetu.
Tunataka Rais ambaye anachukua hatua kwa kufuata katiba, sheria, kanuni na utaratibu (due process) baada ya uchunguzi kukamilika na hakuna anayeonewa.
Wafanyakazi wa NAOT ni wanadamu na hivyo wanaweza kukosea hapa na pale.
Kama tunataka Rais wetu apate kile anachokitaka kutoka kwenye ripoti hizi na sisi wananchi tuendelee kuwa salama kwa sababu ya kuwa na Mkuu wa Nchi anayependa kufuatwa kwa taratibu zote, ni muhimu kuacha michakato iende mpaka mwisho.
Lakini katika yote, tusisahau jambo moja katika mijadala yetu, kwamba kama tumefurahi kuwa ripoti ya CAG imeshiba taarifa na inatoa picha halisi ya mahali tulipo kwenye uwajibikaji wa mali ya umma, tujue kwamba kuna mkono wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye hilo.
Historia inatuonesha kuwa asili ya ripoti ya CAG ni kufichua madudu. Kwa vile watumishi wa umma ni wanadamu, jambo hilo halitabadilika. Kitakachobadilika ni Rais.
Kwa sababu hiyo, ni muhimu kutambua bahati tuliyonayo sasa ya kuwa na Rais anayetaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali atimize majukumu yake,.
Mwisho
Post a Comment