Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu Ester Midimu ametoa kiasi cha shilingi mil. 43.5 kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi Umoja wa Wanawake (UWT) mkoani humo.
Amesema anatoa fedha hizo ili kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi kwa kuendeleza mitaji na biashara zao ndogondogo ikizingatiwa kuwa wanawake ni walezi wa familia na wanachangia uchumi na pato la taifa.
Akizungumza na Wajumbe wa UWT wilaya ya Bariadi jana, katika kikao kilichofanyika ukumbi wa CCM mjini Bariadi, Ester amesema kuwa ametoa fedha hizo kwa kila wilaya ili kumuunga mkono Rais Samia katika kuwezesha na kuwakwamua wanawake kiuchumi.
Amewataka wanawake hao kuyatangaza mema na mazuri yanayotekelezewa na Rais Samia, Mbunge wa jimbo la Bariadi Mhandisi Kundo pamoja na Madiwani kwenye miradi ya maendeleo ambapo kila kata kuna mradi wa maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji, barabara au umeme.
‘’Rais Samia anatujali watanzania, kazi zinaendelea kutekelezwa kila mahali…twendeni kila kata na matawi tukayaseme mazuri ya Rais Samia sababu anafanya miradi ya maendeleo nchi nzima, nami namuunga mkono kwa kuwawezesha wanawake mitaji’’ anasema Ester.
Amesema maendeleo yamekuja kwa kasi katika mkoa wa Simiyu hususani wilaya ya Bariadi huku akiwaomba jumuiya hiyo kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025.
‘’Najua Bariadi ni wachapa kazi, naelewa biashara na vikundi vyenu, natoa mil. 8.5 ili mkaendeleze biashara zenu na kwa mkoa mzima nimetoa mili 43.5 ili wanawake mkafanye biashara ndogondogo’’ amesema Midimu.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Simiyu Mariam Manyangu aliwataka wanawake hao kutumia vizuri fedha walizopewa ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuendeleza mitaji yao.
Aliwataka kufanya kazi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na za UWT ili serikali ya CCM chini ya Rais Samia iendelee kukaa madarakani na wao waendelee kuserebuka.
Fikiri James kutoka kata ya Ngulyati amemshukuru Mbunge huyo kwa kuwawezesha kiuchumi kwani amewapatia mitaji kwa ajili ya kuendeleza biashara zao.
Amewataka wanawake hao kwenda kutumia ipasavyo fedha hizo ili ziweze kuwasaidia na familia zao kwa kukuza uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
Katika kuwezesha UWT, Mbunge Midimu ametoa shilingi mil. 12 (Maswa), mil. 10 (Itilima), mil. 9 (Meatu), mil. 8 (Bariadi) na mil. 4.5 (Busega) na kufanya jumla ya shilingi mil. 43.5.
MWISHO.
Post a Comment