Wanafunzi waonywa kujihusisha na Mapenzi shuleni.

WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Sukuma wilayani Maswa mkoani Simiyu.

 


Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) na MNEC Zainabu Shomari amewataka wanafunzi hususani wasichana kusoma kwa bidii kutoka na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia kuwajengea miundombinu mizuri ya elimu ikiwemo madarasa, maabara na matundu ya vyoo.

 

Ameyasema hayo leo mara baada ya kukagua vyumba vinne vya madarasa vilivyojengwa katika shule ya sekondari Sukuma kwa gharama ya shilingi milioni 80.

 

Amesema Rais Samia ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, hivyo wanafunzi wanao wajibu wa kusoma kwa bidii na kwamba shule za serikali zimekuwa zikifanya vizuri kuliko shule binafsi.

 

‘’Kuna Haki na Wajibu, serikali imetimiza wajibu wake, hivyo ni haki yenu kusoma kwa bidii na kufaulu hasa wanafunzi wa kike…wanafunzi wanaanza kidato cha kwanza au cha tano wengi lakini wanamaliza wachache, niwaombe msome kwa bidii’’ amesema.

 

Amesema lengo la serikali kujenga miundombinu ya elimu ni kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri ili kupata wataalamu wa baadae huku akiwataka wanafunzi hao kuwaheshimu walimu wao.

 

‘’Mmekuja kusoma, mengine hayawahusu…hauruhusiwi kujihusisha na mapenzi katika umri wa shule sababu utapata mimba za utotoni na kuzima ndoto za kupata elimu, mawazo na fikra yakae katika elimu’’ amesema.

 

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohamed amesema wananchi wameona namna Rais Samia anavyopenda elimu kwa kuendelea kujenga miundombinu ya elimu.

 

Amesema hadi sasa kila eneo yamejengwa madarasa mazuri ili wanafunzi wasome katika mazingira rafiki na kuondoa hali ya kuchangishana iliyokuwepo huko nyuma.

 

Awali Mkuu wa Shule ya Sekondari Sukuma Lucas Mazoya amesema mradi wa vyumba vinne vya madarasa umetekelezwa na serikali kuu na umewapunguzia msongamano wanafunzi madarasani pia kuongeza hali ya ufundishaji na ujifunzaji.

 

Amesema mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya shilingi mil. 80 ili kuwekeza kwenye elimu ili ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023 wanafunzi wote wanaochaguliwa wajiunge wote kidato cha kwanza.

 

MWISHO.

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) na MNEC Zainabu Shomari (katikati) akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohamed pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari Sukuma wilayani Maswa.

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) na MNEC Zainabu Shomari (wa tatu kushoto) akimsikiliza Diwani wa Kata ya Sukuma Mary Misangu, mara baada ya kukagua vyumba vinne vya madarasa shule ya sekondari Sukuma, kushoto ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu.

 

 

Diwani wa Kata ya Sukuma Wilayani Maswa Mkoani Simiyu Mary Misangu (wa pili kushoto) akiongea mara baada ya Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) na MNEC Zainabu Shomari kukagua ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, kushoto ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa ISmiyu Shemsa Mohamed.
 
 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Maisha Mtipa (wa kwanza kulia) akiongea mara baada ya Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) na MNEC Zainabu Shomari kukagua ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa shule ya sekondari Sukuma, kushoto ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu Shemsa Mohamed.
 
 




 

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post