Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) zimeibua mjadala mkubwa na mpana nchini tangu zitolewe hadharani siku chache zilizopita.
Ripoti hizo za mwaka wa fedha wa 2021-2022 zimeweka bayana kasoro mbalimbali kwenye serikali kuu, tawala za mikoa na serikali za mitaa pamoja na mashirika ya umma.
Kasoro hizo ni pamoja na tuhuma za ubadhirifu wa pesa za umma na uendeshaji wa hasara wa baadhi ya mashirika ya umma.
Lakini, mambo yaliyoibuliwa na ripoti hizi mpya za CAG siyo mapya na siyo ishara ya kuongezeka kwa ufisadi nchini.
Mfuatiliaji yoyote makini wa ripoti za CAG atabaini kuwa mambo yaliyoibuliwa kwenye ripoti za mwaka huu yamekuwa yakiibuliwa pia kwenye ripoti za awamu zilizotangulia kwa miaka kadhaa sasa.
Kuna tofauti kuu saba zifuatazo kati ya mazingira ya utoaji wa ripoti za CAG chini ya Awamu ya Tano na utoaji wa ripoti za CAG kwenye Awamu hii ya Sita:
1. Kuongezeka kwa uhuru wa CAG
Tangu aliyekuwa CAG, Profesa Mussa Assad, kung’olewa kazini na utawala wa Awamu ya Tano kinyume na katiba kwa kusema ukweli na kusimamia kile anachokiamini, ofisi ya CAG imekosa uhuru wa kufanya kazi yake, hadi ilipoingia madarakani Serikali ya Awamu ya Sita na kurejesha uhuru huo kwa CAG.
Kwenye awamu iliyopita, CAG hakuwa na uhuru wa kukagua na kutoa ripoti za miradi ya kimkakati ya maendeleo, ikiwemo reli ya SGR, ununuzi wa ndege za ATCL, TTCL na ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa JNHPP, tofauti na sasa kwenye Awamu ya Sita ambapo amepewa uhuru kufanya ukaguzi na kubaini kasoro kadhaa kwenye miradi hiyo.
2. Kuongezeka kwa uhuru wa vyombo vya habari
Uhuru wa habari umeimarika kwenye Awamu ya Sita na kuvipa vyombo vya habari fursa ya kuripoti tuhuma zilizoibuliwa na CAG bila woga wa kufungiwa au kushughulikiwa na watu wasiojulikana.
Maana yake ni kwamba, maudhui yaliyomo kwenye ripoti za CAG yameripotiwa kwa uzito mkubwa na vyombo vya habari tofauti na hali ilivyokuwa chini ya Awamu ya Tano, ambapo wanahabari waliogopa kuripoti taarifa hizo.
3. Kuongezeka kwa uhuru wa vyama vya upinzani
Awamu ya Sita imerejesha uhuru wa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, na hiyo imewapa fursa viongozi wa upinzani kuzunguka nchi nzima kuzungumzia ripoti za CAG kwenye majukwaa ya siasa na hivyo basi kusambaza mjadala huo kila kona ya nchi.
Kiongozi mmoja wa chama kimoja cha upinzani alisikika akisema juzi kwenye mkutano wa hadhara kuwa angekuwepo aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, wote waliotajwa kwenye ripoti za CAG “wasingekuwepo.”
Kauli hiyo imewashangaza hata wafuasi wa chama hicho, kwani kiongozi huyo huyo wa upinzani alikimbia nchi kusalimisha maisha yake kwenye utawala wa Awamu ya Tano na mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani ilipigwa marufuku, ambapo asingeweza kuwa na jukwaa la hadhara la kuzungumzia ripoti za CAG.
4. Kuongezeka kwa uhuru wa wanaharakati
Taasisi zisizo za kiserikali pamoja na wanaharakati wamepata uhuru zaidi kwenye Awamu ya Sita kuzungumzia mambo mbalimbali, ikiwemo ripoti za CAG, tofauti na hali ilivyokuwa kwenye awamu iliyopita.
5. Kuongezeka kwa uhuru wa wabunge wa CCM
Wabunge wa chama tawala, ambao kwenye awamu iliyopita walizibwa mdomo na hawakuwa na uhuru wa kuikosoa serikali ndani na nje ya Bunge, sasa wanatumia uhuru wao chini ya Serikali ya Awamu ya Sita kupaza sauti zao juu ya kasoro zilizotajwa na CAG.
6. Kuongezeka kwa uhuru wa wastaafu
Viongozi mbalimbali wastaafu ambao kwenye Awamu ya Tano waliambiwa wakae kimya waache “kuwashwa washwa” sasa hivi wana uhuru wa kuongea, kushauri na hata kuikosoa serikali bila hofu yoyote.
7. Kuongezeka kwa uhuru wa kuongea wa wananchi
Tofauti na hali ilivyokuwa kwenye Awamu ya Tano ambapo wananchi walikosa uhuru wa kuongea na kuikosoa serikali, wananchi sasa wamerejeshewa uhuru huo chini ya Awamu ya Sita na wanautumia kujadili ripoti za CAG kwa uwazi bila woga.
Wachambuzi wa masuala ya utawala wanasema kuwa uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kurejesha tunu za taifa za uhuru na haki kwa kiasi kikubwa utachochea utulivu wa kisiasa na maendeleo endelevu nchini.
Mjadala unaoendelea wa ripoti za CAG umedhihirisha kuwa kilichozidi nchini siyo ufisadi wala uendeshaji mbovu wa mashirika ya umma, bali kilichozidi kwenye Awamu ya Sita kulinganisha na awamu iliyopita ni uhuru. Na hili ni jambo jema sana kwa mustakabali wa taifa letu.
إرسال تعليق