Na COSTANTINE MATHIAS, Itilima.
WIZARA ya Afya imesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza Bajeti ya dawa katika Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu kutoka mil. 127 mwaka 2021 na kufikia mil. 511 mwaka 2022.
Aidha imeelezwa kuwa katika bajeti iliyopitishwa mwaka huu 2023, Rais Samia ameongeza fedha za dawa katika wilaya hiyo na kufikia kiasi cha shilingi milioni 795.
Hayo yamebainishwa leo na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akiongea na watumishi wa afya wilayani humo alipokuwa akikagua shughuli za utoaji wa huduma kwenye zahanati, vituo vya afya na Hospitali ya wilaya.
Waziri Ummy amewataka watumishi wa afya kuhakikisha dawa zinapatikana hospitalini ili wananchi waweze kunufaika na fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kuwahudumia.
‘’Rais ameshamaliza wajibu wake, sisi wasaidizi wake na watumishi wa afya tuhakikishe dawa zinapatikana kwenye vituo vya kutolea huduma…tunatakiwa kufanya maoteo sahihi, tulete mfamasia hapa ili aweze kusadia kufanya kazi’’ amesema Waziri Ummy.
Amefafanua kuwa katika mkoa wa Simiyu, Rais Samia ameongeza fedha za dawa kutoka bil 3.9 na kufikia bil. 5 katika bajeti iliyopitishwa mwaka huu 2023/24.
Amewataka watumishi wa afya kuhakikisha wanaagiza dawa kwa wakati kwa kuzingatia magonjwa muhimu yanayopatikana eneo hilo, pia kusimamia matumizi sahihi ya dawa.
Ameitaka pia Halmashauri hiyo kuajiri mtaalamu wa muda wa mionzi ili aweze kufanya kazi kwenye chumba cha X-ray ambacho hakina mtaalamu licha ya vifaatiba kuwepo.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito, huku akiwataka watumishi wa afya kuendelea kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu ili waweze kupatiwa matibabu.
Mbunge wa Jimbo la Itilima Njalu Silanga ameiomba wizara ya Afya kuendelea kuajiri watumishi wa afya kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa wananchi vijijini.
Amesema wilaya hiyo imekamilisha ujenzi wa zahanati 10 ambazo zimekosa usajili kwa kigezo cha kutokuwa na nyumba za watumishi.
Ameiomba serikali kuzisajili haraka zahanati hizo ili zianze kutoa huduma kwa wananchi wakati halmashauri ikikamilisha ujenzi wa nyumba za watumishi kwa utaratibu uliowekwa.
Awali Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Itilima Dkt. Emmanuel Costantine amesema wamekamilisha ujenzi wa majengo Hospitali katika kijiji cha Nguno yaliyogharimu shilingi bil. 3.1.
Amesema wamekamilisha jengo la wagonjwa wa nje (OPD), mionzi, jengo la dawa, utawala, maabara, jengo la wazazi,wodi ya wanaume, wanawake na watoto, upasuaji, jengo la dharura na la kuhifadhia maiti.
Ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za afya licha ya kukabiliwa na upungufu wa watumishi, nyumba za watumishi na ukosefu wa njia ya kupitisha wagonjwa.
MWISHO.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akisoma na kupitia taarifa ya hali ya utoaji wa huduma ya afya wilayani Itilima Mkoani Simiyu, alipofanya ziara ya kikazi leo.
إرسال تعليق