Mitambo ikifanya kazi ya kupakia Pamba kwa ajili ya kuchakatwa katika kiwanda cha Alliance Ginnery kilichopo Kasoli wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
CHAMA cha Wanunuzi wa Pamba nchini Tanzania (TCA) kimeiomba serikali kwa kushirikiana na viongozi wa Vijiji kudhibiti wakulima wanaochafua pamba kwa lengo la kuongeza uzito.
Wamesema endapo wataendelea kuchafua pamba hiyo, watakosa soko na watauwa mbegu ambazo hurudishwa kwa wakulima kwa ajili ya kupanda msimu unaofuata na pia vipuri vya mashine na mitambo inaharibika kwa haraka.
Hayo yalibainishwa na Katibu wa Chama hicho, Boaz Ogolla wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo aliiomba serikali kwa kushirikia na wadau wa Pamba kuendelea kutoa elimu kwa wakulima na wanunuzi ili wazingatie ubora.
Amesema hivi karibuni kuna baadhi ya wakulima wanauza pamba iliyochanganywa Maji na mchanga ili kuongeza uzito, hali inayosababisha kukataliwa ili inanikwe juani na kuchambuliwa ili kuondoa uchafu.
‘’Wanunuzi ambao ni vyama vya ushirika (Amcos) na wanunuzi binafsi, wananunua pamba ambayo haina ubora ikabidi tuianike juani ili ikaushwe…Mwaka jana na mwaka juzi hili lilidhibitiwa sana, tunajaribu kuelimisha wanunuzi wa pamba na viongozi watusaidie kutoa elimu’’ amesema.
Ogolla ambaye pia ni Meneja wa Kiwanda cha Pamba cha Alliance Ginnery ameipongeza serikali kwa kuendelea kusimamia bei ya pamba ili isishuke, huku akiwatoa hofu wakulima kuwa soko la kimataifa na soko la mbegu halipo kutokana na soko la mafuta kushuka.
Amewataka wakulima kuuza pamba mapema kwa sababu hawajui baadae kama bei ya pamba itashuka au kupanda huku akiwahakikishia kuwa wanunuzi wamejipanga kununua pamba yote kutoka kwa wakulima vijijini.
Amesema hadi sasa kampuni hiyo, wamenunua kilo milioni 15 huku lengo lao ni kupata kilo milioni 30 na uzalishaji umeongezeka tofauti na mwaka jana ambapo sekta nzima ya pamba nchini walipata kilo milioni 175.
Ofisa Ufuatiliaji na Uhamasishaji kutoka Bodi ya Pamba Edward Nyawile amesema hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kwa vyama vya ushirika na wanunuzi wa pamba wanaochafua zao hilo.
Amezitaja hatua hizo endapo watabainika ni pamoja na kufungiwa kituo cha ununuzi wa Pamba, au kupigwa faini ya shilingi laki tano na kiwanda kikipokea Pamba chafu wanapigwa faini ya dola 1,000 au kufungiwa kufanya kazi.
Amesema wakaguzi wa Pamba wa wilaya wanaendela kutoa elimu na kupita kwenye vituo vya kununulia Pamba na viwandani kwa ajili ya ukaguzi huku akiitaja wilaya ya Bariadi kushamiri kwa uchafuzi wa Pamba.
MWISHO.
إرسال تعليق