Waziri Ummy asisitiza Uwajibikaji Watumishi wa Afya


 WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu akiongea na Watumishi wa Idara ya Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu iliyoko Nyaumata, Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

 

Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.

 

WIZARA ya Afya imewataka Watumishi wake kuhakikisha wanaimarisha utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa baada ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu kutimiza wajibu wa kujenga miundombinu ya afya ikiwemo Zahanati, Vituo vya afya, Hospitali za Wilaya, Mikoa na Rufaa.

 

Aidha watumishi hao wametakiwa kuzingatia weledi na miongozo ya Wizara ya Afya katika utoaji wa huduma kwa wananchi huku wakionywa juu ya matumizi ya lugha chafu na kwamba wizara hiyo haitawafumbia macho.

 

Hayo yamebainishwa leo na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipofanya ziara ya kikazi na kuzungumza na watumishi wa afya mkoani huo ambapo amesema serikali imetimiza wajibu wake ambapo wananchi wanahitaji huduma bora za matibabu.

 

Amesema katika sekta ya afya, serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya vifaa tiba, ujenzi wa miudombinu ikiwemo majengo ya kutolea huduma za afya na kuongeza watumishi wa afya ambapo watumishi wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili.

 

‘’Rais Samia ametimiza wajibu wake, wananchi wanahitaji huduma bora za afya, hili la utoaji wa huduma bora siyo la Rais Samia ni la kwetu…kama kuna changamoto zozote za wana Simiyu kwamba hawapati huduma bora za afya, Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala na watendaji wengine tunatakiwa kuwajibika’’ amesema Waziri Ummy.

 

Amewataka watumishi hao kuhakikisha wanamsaidia Rais Samia ili wananchi wa Mkoa wa Simiyu wapate huduma bora za afya, huku akionya kuwa watumishi wengi wa sekta ya afya wamekuwa wanajali sana semina kuliko kutoa huduma kwenye vituo.

 

Amesema kwa sasa serikali ya awamu ya sita haizungumzii idadi ya majengo na ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali bali wanataka kuona utoaji wa huduma bora kwa wananchi ambapo watumishi wengi watapimwa kwa utendaji.

 

‘’Madaktari wafanye kazi za utoaji wa huduma kwa kuzingatia maadili na weledi, utoaji wa lugha chafu kwa wagonjwa…idara ya afya zingatieni maadili na weledi kwenye taaluma yenu’’ amesisitiza Waziri Ummy.

 

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa kuimarisha huduma za afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto ambapo amefafanua kuwa kipaumbele cha Rais Samia ni kuimarisha huduma ya afya ya Mama na Mtoto.

 

MWISHO.

 

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda (kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati wakiongea na Watumishi wa Idara ya afya mkoani humo.

 

 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Boniface Marwa akiwasilisha taarifa ya utoaji wa huduma ya afya katika mkoa huo, mbele ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu (hayupo pichani).

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم