Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu amewataka Wazazi, Walezi, Jamii, Viongozi wa madhehebu ya Dini, Serikali na Vyama vya Siasa kuungana kwa pamoja kupiga vita matendo ya Ushoga na Ulawiti ambayo yameanza kushamiri katika jamii.
Aidha, Sangu amesema vitendo hivyo ni kinyume na mapenzi ya Mungu na pia ni uvunjifu wa haki za kibinadamu na kwamba wanaoshabikia utamaduni huo haupo katika mila za Kitanzania na Kiafrika.
Ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akiendesha Ibaada za Misa katika Kigango cha Mbiti na wakati wa utoaji wa kipaimara kwenye Parokia na Mtakatifu Barkita Ngulyati wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Sangu amesema Utamaduni wa Ushoga na Ulawiti haupo katika mila za kiafrika na kitanzania ikiwemo kabila la kisukuma huku akiwataka waumini kulinda tunu za ndoa.
‘’Mila na destruri za kisukuma hakuna kitu kama hicho, utaonekana ni taahila na umepungukiwa…tulinde tunu za ndoa, wajibu wetu kama wazazi katika familia zetu tupige vita ushoga na ukimwona mtoto anatembea kinamnanamna lazima ujiulize maswali’’ amesema Askofu Sangu.
Amesema katika maandiko ya dini, Mwenyezi Mungu aliwabariki mwanamke na mwanaume na kusema zaeni mkaongezeka, mkaitawale nchi, hivyo ni wajibu wa jamii kufanya hivyo kwa nguvu ya roho mtakatifu.
Amesema bila uwezo wa nguvu ya roho mtakatifu, binadamu hawana uwezo na pia ni wadhaifu na kwamba ni Mungu roho Mtakatifu anafanya kazi ndani ya nafsi za watu kupitia matukio mbalimbali ya kiimani.
‘’Mapendo ya kimungu, ni mapendo yanayohusisha nafsi na ubinafsi kwa ajili ya Mungu na jirani, tunahitaji sadaka kufikisha nafsi na ubinafsi kwa ajili ya jirani…na upendo ni kuwasemea wenzetu yaliyo mema, siyo chuki, masengenyo, fitina , mafarakano…kuwatendea na kuwasemea wenzetu yaliyo mema’’ amesema Sangu.
Amewataka watu kupenda kwa sababu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu, kwani Mungu alimuumba mtu kwa sura na mfano wake ambapo wanapaswa kutendeana na kusemeana yaliyo mema.
MWISHO.
Post a Comment