MBUNGE MASHIMBA ACHANGIA SHILINGI MIL.10 SACCOS YA UVCCM MASWA MAGHARIBI


Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi kiasi cha Sh Milioni 10 katika Saccos ya Vijana wa CCM katika jimbo hilo.


Na Samwel Mwanga, Maswa


MBUNGE  wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki, ametimiza ahadi yake kwa vijana wa jimbo hilo kwa kutoa mchango wa Sh Milioni 10 kwa SACCOS ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)jimbo la  Maswa Magharibi.


Mchango huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya jitihada za mbunge huyo kuunga mkono juhudi za vijana katika kujikwamua kiuchumi kupitia miradi ya ujasiriamali na maendeleo ya kijamii.


 Akizungumza Mei 22,2025  mjini Malampaka wilayani  Maswa katika hafla fupi wakati wa kukabidhi risti ya benki ambayo ni ushahidi wa kuweka fedha hizo kwenye akaunti ya benki ya Saccos hiyo mbunge Ndaki alisisitiza dhamira yake ya kuwawezesha vijana kuwa chachu ya maendeleo na kuahidi kuendelea kushirikiana nao kwa karibu katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo.


“Ninayo furaha leo kutimiza ahadi niliyotoa kwa vijana wetu wa Umoja wa Vijana wa CCM katika jimbo letu la Maswa Magharibi ,natambua mchango mkubwa wa vijana katika ujenzi wa taifa letu, na ninaamini kuwa kupitia SACCOS hii, wataweza kupata mitaji ya kuanzisha au kukuza shughuli zao za kiuchumi,” amesema.


Amesema kuwa pamoja na kutoa fedha hizo atatafuta na wadau wengine ili waweze nao kuchangia  hivyo ni vizuri zikatunzwa na kutolewa kama mikopo kwa kufuata taratibu na kanuni ambazo wamejiwekea na si vinginevyo.


“Niwaombe vijana Saccos fedha hii niliyowapa kama mtaji hakikisheni mnaitoa kwa kukopeshana kwa kufuata kanuni na taratibu ambazo mmejiwekea pia katika kutoa mikopo ni lazima muangalie watu ambao mnawakopesha ambao wanashughuli zao kama vile biashara ili waweze kurejesha kwa wakati na wengine wakope,”amesema.


Pia amesisitiza vijana watakaochukua mkopo wa fedha katika Saccos hiyo wakazitumie kwa manufaa ya kuendeleza shughuli zao mbalimbali za kiuchumi na siyo kwenda kufanyia starehe.


Katibu wa CCM wilaya ya Maswa,Efreim Kolimba ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo pamoja na kumpongeza mbunge huyo kwa kutimiza ahadi hiyo amesema kuwa kuanzishwa kwa Saccos hiyo ni kuwakomboa kiuchumi vijana wa chama hicho katika jimbo hilo.


“Hii Saccos ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 na lengo lake ni kuwakomboa vijana wa jimbo hili wa CCM ili waweze kuinua vipato vya kila mmoja binafsi na haitatumika kisiasa na sisi tupo kwa ajili ya kusimamia ila mamlaka yote yapo kwa Vijana wa CCM jimbo hili,”amesema.


Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Maswa,Haji Kwizombe amesema kuwa jambo ambalo limefanywa na mbunge huyo ni la kizalendo kwa vijana wa chama hicho wa jimbo hilo na linafaa kuigwa na wabunge wengine kwa kuwathamini vijana ambao wamekuwa wakifanya nao kazi mbalimbali ndani na nje ya chama.


“Hili jambo lililofanyika hapa naamini linakwenda kuwa chache nchi nzima nadhani huyu ndiye mbunge wa kwanza kulifanya hapa nchini nawaomba na viongozi wengine kuwawezesha vijana katika maeneo yao ili waweze kujiinua kiuchumi wao kama alivyofanya mbunge Mashimba Ndaki kwa vijana wa jimbo lake la Maswa Magharibi,”amesema.


Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Saccos hiyo,Shola Joseph pamoja na kumshukuru mbunge huyo kwa kutoa mchango wake huo na kuhahidi kuzitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa hususan katika kuwawezesha wanachama wao kupitia mikopo yenye masharti na riba nafuu.


Veronika Ntobi ni Katibu UVCCM kata ya Malampaka amesema kuwa ni vizuri vijana kujitokeza na kuwa wajasiliamali ili waweze kupata mikopo kwa ajili ya kufanyia shughuli mbalimbali za uzalishaji na kuepuka mikopo ile ya kausha damu.


Naye Patrick Pauline ambaye ni Katibu Uhamasishaji na Chipukizi Kata ya Sengwa wilayani humo amesema kuwa utaratibu wa Saccos yao utakuwa wa riba nafuu maana ukikopa Sh 100,000/-riba yake kwa mwezi ni Sh 5,000/-hivyo ni vizuri kwa vijana kuchangamkia fursa hiyo kuliko kujiingiza kwenye mikopo yenye riba kubwa.


Mchango huu unakuja wakati taifa linaendelea kuhamasisha ushiriki wa vijana katika shughuli za maendeleo, hasa katika maeneo ya vijijini ambapo changamoto za ajira na mitaji bado ni kubwa.


Mwisho.


Katibu CCM wilaya ya Maswa, Efreim Kolimba akizungumza wakati wa hafla ya mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki kukabidhi kiasi cha Sh Milioni 10 katika Saccos ya Vijana wa CCM katika jimbo hilo.

Sehemu ya wanachama wa Saccos ya Uvccm Jimbo la Maswa Magharibi wakati wa hafla kukabidhiwa fedha sh Milioni 10 zilizotolewa na mbunge wa jimbo hilo, Mashimba Ndaki.








Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post