Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Simiyu imedhibiti upotevu wa zaidi ya shilingi milioni 300 kwa kuzuia mnada wa haramu wa ghala na nyumba tatu zilizokuwa zikiuzwa mjini Bariadi.
Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake, Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo Aron Misanga amesema mnada huo uliendeshwa na kampuni ya Bani Investment Ltd katika mazingira yanayoashiria ukiukwaji wa taratibu na uwepo wa vitendo vya rushwa kwa watendaji waliohusika na utoaji wa vibali.
Amefafanua kuwa, mnada huo ulikuwa unahusisha mali za mfanyabiashara aitwaye Sibu Nsungi Manabu, msukuma na mkulima mkazi wa Bariadi mjini ambaye alikuwa amekopa kwenye Benki moja mjini humo.
‘’katika huo mkopo na taratibu zao, mnada ulikuwa ufanyike ili kurejesha mkopo huo…lakini ili mnada ufanyike kuna taratibu zake zinatakiwa zifanyike ikiwemo kuhusisha vyombo vya serikali ikiwemo halmashauri kutoa vibali’’ amesema.
Ameeleza kuwa Taasisi hiyo ilifuatilia ili kubaini kama taratibu za kisheria zimezingatiwa na kubaini kuwa kulikuwa na mnada uliokuwa ikiendeshwa na Bani Investment lakini kulibanika mazingira ya Rushwa na ukiukwaji wa taratibu.
Amesema baada ya kuingilia kati, walibaini kuwa katika mnada huo kulikuwa na ghala lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500 ambalo lilikusudiwa kuuzwa kwa bei chini ya shilingi 200 na ilitarajiwa baada ya kuuza ghala wauze pia nyumba tatu za mmiliki huyo.
Ameongeza kuwa baada ya Taasisi hiyo kuona hivyo, walifanya kazi ya kuzuia ili haki na taratibu ziweze kufuatwa na kwamba kwa wakati huo mnada haukuweza kufanyika.
MWISHO.
Nyumba ya makazi iliyoko mtaa wa Butiama mjini Bariadi iliyotaka kupigwa mnada kinyume na utaratibu.
إرسال تعليق