Na Derick Milton.
Kesi ya Jinai Na 08 ya mwaka 2023 iliyokuwa
inamkabili Askari wa Jeshi la Polisi H.4178 Abati Benedectio wa kituo Cha Polisi
Bariadi mkoani Simiyu kutuhumiwa kumpiga hadi kumjeruhi vibaya mtoto
wake mwenye umri wa miaka 7 (jina linahifadhiwa) imerejeshwa tena.
Askari hiyo Februari 17, 2023 alifikishwa katika Mahakama ya
Wilaya ya Bariadi, kujibu tuhuma zilizokuwa zinamkabili, ambapo baadaye
ilifutwa Mei 22, 2023 kwa madai kuwa mashahidi upande wa Jamhuri kushindwa
kufika Mahakamani mara tatu mfululizo.
Kabla ya kufutwa, Askari huyo alisomewa Mashtaka mbele ya
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Mariamu Nyangusi na mwensesha Mashitaka wa
serikali kwa wakati huo Daniel Masambu.
Masambu alieleza kuwa mtuhumiwa alimchapa mtoto wake kwa
fimbo na kumjeruhi maeneo mbalimbali ya mwili wake kinyume na kifungu Cha 169 A
kifungu kidogo Cha 1 na Cha 2 Cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura 16
marejeo ya mwaka 2022.
Kesi hiyo ilifutwa kwa kile kilichoelezwa kuwa mashahidi
kushindwa kufika makamani mara tatu mfululizo kutoa ushahidi.
Majibu ya kuwa mashahidi hao hawapo yalitolewa na Jeshi la
Polisi upande wa upelelezi katika Ofisi ya Mashitaka mkoa baada ya kupelekewa
hati tatu za kuitwa shaulini (Samas) mashahidi watatu ambao walikuwa ni Mtoto
mwenyewe, Mama mzazi wa mtoto pamoja na mama Mlezi wa mtoto.
Ofisi ya Mashitaka ilieleza kuwa Hati zote 3 zilijibiwa na
jeshi la polisi, kuwa mashahidi wanaohitajika hawapo Bariadi na hawajulikani
walipo, ndipo kesi ikafutwa.
Hata hivyo sababu hizo zilionekana kuwa hazina ukweli, kwani
mashahidi wote waliokuwa wanahitajika walikuwa wanapatikana na wanaishi mjini
Bariadi ambapo baadhi ya mashahidi hao walisema hawajawahi kupata barua ya wito
kuwa wanahitajika mahakamani.
Kesi yarejeshwa
tena.
Leo Kesi hiyo imerudishwa tena ikiwa imepita miezi mitatu
tangu kufutwa ambapo imekuja kama kesi mpya Jinai Namba 59, 2023 na wameanza kusikilizwa
mashahidi wa upande wa Jamhuri.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Caroline Kiliwa
wamesikilizwa mashahidi wawili kati ya tisa watakaotoa ushahidi, ambapo leo
waliotoa ushahidi ni mtoto mwenyewe pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha
Polisi Bariadi wakati huo SSP Piter Ntinginya.
Baada ya kusikilizwa kwa Mashahidi hao, Hakimu amehairisha
kesi hiyo hadi Oktoba 12, 2023 kesi ikapoendelea kusikilizwa tena.

Post a Comment