Ridhiwani aridhishwa na Utekelezaji wa Miradi ya TASAF Simiyu.

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Ridhiwan Kikwete (aliyenyoosha kidole) akikagua ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa afya iliyojengwa na TASAF katika zahanati ya Mbiti.
 


Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.

 

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Ridhiwan Kikwete amesema ameridhishwa na Utekelezaji wa Miradi ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) huku wanufaika wake ni wananchi wasiokuwa na uwezo.

 

Aidha amesema miradi ya TASAF ni tofauti na miradi mingine ya serikali kwa sababu inaonekana kwa macho na utekelezaji wake unawagusa wananchi waishio vijijini moja kwa moja.

 

Ridhiwani ameyasema hayo leo kwenye wakati akiongea na watumishi wa serikali mkoani humo pamoja na kutembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF III).

 

Amesema Utekelezaji wa miradi ya kupunguza Umaskini (TPRP) kupitia Mpango wa Kunusu Kaya Maskini, umefanikiwa kutokana na mipango mizuri ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia ambapo zaidi ya Bil. 9.2  zimetolewa katika mkoa wa Simiyu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

 

‘’TASAF wana Uwezo wa kuzisimamia hizo fedha, kama hakuna uwezo wa kuzisimamia, tutaishia kugombana tu, tunachotaka tukileta fedha tuone thamani halisi ya fedha hizo…hivi ndivyo miradi inavyotakiwa kufanyika’’ amesema Ridhiwan.

 

Amezitaka Halmashauri kujifunza kwenye miradi ya TASAF ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa wakati na kuleta tija kwa wananchi na inatekelezwa na watu wanaotaka matokeo yanayooneka.

 

Amefafanua kuwa moja ya kundi kubwa linalonufaika na miradi ya TASAF ni kaya maskini ambazo hazina uwezo wa kulipia watoto mahitaji ya shule, uhakika wa kupata matibabu na chakula.

 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amewataka watendaji wa TASAF kuangalia namna ya upatikanaji wa asilimia 10 inayochangiwa na wananchi wakati wa utekelezaji wa miradi kwenye jamii.

 

Amesema maagizo ya Rais, ni kulenga mafanikio na utumishi wa umma ulio bora lazima uwe na mipango ya kutambua mteja na mnufaika wa mpango huo ambapo baadhi ya wananchi wanashindwa kuchangaia asilimia 10 kutokana na hali duni za maisha yao.

 

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda ameipongeza serikali kwa kubadili mfumo wa malipo kwa walengwa ambapo huko nyuma waliwakuwa wanapokea njia ya simu na benki na kwamba wananchi wengi walikuwa hawapati malipo kwa wakati.

 

Amesema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) unahusisha wananchi wa hali ya chini sana ikiwemo wazee ambao hawana uwezo wa kutumia mifumo ya kibenki ikiwemo simu hali ambayo ilikuwa inasababisha changamoto ya kukosa malipo yao.

 

Aidha, Dk. Nawanda amesema wananchi wanapata changamoto ya uchangiaji wa asilimia 10 ya miradi ya TASAF, jambo ambalo linakwamisha utekelezaji wa miradi kwa wakati kutokana na wananchi kukosa fedha au uhaba wa nguvu kazi.

 

Awali Mratibu wa TASAF Mkoa wa Simiyu Nyasilu Ndulu amesema wanatekeleza miradi ya kuondoa umaskini awamu ya nne (TPRP IV) ambapo jumla ya shilingi Bil. 9.2 zimepokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Afya, Elimu na kukuza uchumi wa kaya.

 

Amesema hadi sasa zaidi ya Bil. 6 zimetumika sawa na asilimia 65, jumla ya kondoo 2947 wenye thamani ya mil. 217.7 wamegawia vikundi 52, mbuzi 459 wenye thamani ya mil. 22.5 katika vikundi 12 na mil. 9.6 zimetumika kununua mizinga 150 na kupewa vikundi 12.

 

 MWISHO.

 

Nyumba ya mtumishi wa Afya katika zahanati ya Mbiti, Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu iliyojengwa na TASAF kwa zaidi ya shilingi mil. 50.
 

Nyumba ya mtumishi wa Afya katika zahanati ya Mbiti, Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu iliyojengwa na TASAF kwa zaidi ya shilingi mil. 50.
 
 
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Ridhiwan Kikwete (mwenye miwani) akipata taarifa kutoka kwa Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji wa Bariadi Omary Masumo (kushoto) wakati akikagua ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa afya iliyojengwa na TASAF katika zahanati ya Mbiti.
 
 
 



Mratibu wa TASAF Mkoa wa Simiyu Nyasilu Ndulu akiwasilisha taarifa ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Mkoani humo namna walengwa walivyonufaika.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda.
 
 
 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post