Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) imewataka
watanzania kujenga tabia ya kuandika wosia, kwani kufanya hivyo itasaidia kwa
kiwango kikubwa kuepusha migogoro ya mara kwa mara kwenye familia na
kuwawezesha warithi halali kupata haki yao kwa wakati.
Akizungumza na waandishi wa Habari Kwenye Kampeini ya
msaada wa kisheria ya Mama Samia ( Mama Samia Legal Aid Campaign) inayoendelea
Mkoani Simiyu Afisa Sheria kutoka RITA Grace Shao ameitaka jamii kuacha woga
kuandika Wosia, kwani kufanya hivyo siyo uchuro na kusema baadhi ya watu
wameandika na wanaendelea kuishi vizuri huku waliondika na wakafariki familia
zao zimeendelea kuishi bila ya migogoro.
“ Familia nyingi zimekuwa na migogoro ya mara kwa mara juu ya
mirathi, wengine wamedhulumiwa na ndugu ambao kisheria siyo waridhi wa mali,
tumeendelea kuwaelimisha wananchi kuwa mwarobaini wa haya ni Wosia,” amesema
Shao.
Aidha Shao amewasihi wananchi kutumia taasisi ya RITA Katika kuandaa wosia kutokana na kuwa chombo cha serikali, lakini pia ni taasisi ambayo haina ukomo wa maisha pamoja na kuwa na wanasheria wabobevu wa masuala ya wosia na mirathi.
Katika hatua nyingine Shao amewahimiza wazazi kujenga tabia ya
kuwatafutia vyeti vya kuzaliwa watoto ili kuondoa usumbufu wanaoweza kupata
pindi watakapotakiwa kwenda kuanza shule na kuhitaji cheti cha kuzaliwa.
Amesema kuwa kwa sasa mtoto akitakiwa kwenda kuandikishwa shule
lazima awe na cheti za kuzaliwa, kupata cheti cha kuzaliwa ni muhimu pia lakini
pia ili mtu apate Bima ya Afya lazima cheti za kuzaliwa awe nacho.
“ Tunawasihi wananchi mtoto akizaliwa ndani ya siku 90 ni muhimu
kumtafutia cheti cha kuzaliwa, hii itasaidia kumtengenezea mtoto msingi mzuri
wa majina yake pamoja na kumbukumbu yake ya tarehe za kuzaliwa” amesema Shao…
“ Kuna changamoto kubwa ya watu majina yao kuwa na shida, utakuta jina la shule ni tofauti na jina kuzaliwa, ikiwa hivyo huyo mtoto atapata shida wakati wa kutafuta kazi, lakini cheti cha kuzaliwa kinapotafutwa mapema inasaidia mtu kuwa na mtiririko mzuri wa majina yake,” ameongeza Shao.
RITA inaendelea Kutoa Huduma ya Usajili na kutoa Vyeti vya vya
kuzaliwa,Elimu ya Mirathi,Kuandika na Kuhifadhi Wosia kwenye Kampeni ya
Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayoendelea kwenye viwanja vya Stendi
ya zamani Mkoani Simiyu
Post a Comment