Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
SERIKALI kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA), Mkoa wa Simiyu imetoa kiasi cha shilingi Bil. 10 kwa ajili ya kutekeleza miradi minne ya Maji katika wilaya za Busega na Itilima.
Aidha katika mwaka wa fedha 2023/24, Wakala huyo ameidhinishiwa kiasi cha shilingi Bil. 32 kwa ajili ya kutekeleza miradi 32 ili kuongeza upatikanaji wa maji Mkoani humo.
Akizungumza jana mara baada ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa miradi ya maji, Meneja wa RUWASA, Mkoa wa Simiyu Mhandisi Mariam Majala alisema mara baada ya mikataba hiyo kusainiwa, wakandarasi watakabidhiwa maeneo ya kazi ndani ya siku saba.
Alifafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24 wameidhinishiwa kutekeleza miradi 32, lakini kwa sasa wamesaini kutekeleza miradi sita na ifikapo mwezi june 2024 miradi yote itakuwa imekamilika.
Akimwakilisha Meneja wa RUWASA wilaya ya Itilima, Mhandisi Hassan Chambale alisema watahakikisha wanawasimamia wakandarasi ili watekeleze miradi ya maji kwa wakati.
Alisema wakandarasi hao wamekidhi vigezo vya kutekeleza miradi hiyo, hivyo wanatakiwa kutekeleza kwa wakati ili wananchi wapate maji safi na salama karibu na maeneo yao.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika Mkoa huo.
Alisema wameshapatiwa zaidi ya shilingi Bil. 31 kwa ajili ya kutekeleza miradi 32 na kwamba wameanza kutekeleza miradi sita katika wilaya za Busega jumla ya vijiji 10 na Itilima vijiji vinne vitapatiwa huduma ya maji.
Aidha katika wilaya ya Busega, Mradi wa Igalukilo na Kalemela utatekelezwa na kampuni ya M/S Ursino Ltd kwa gharama ya shilingi Bil. 3.7, wakati huo Mradi wa Kabita awamu ya pili utatekelezwa na Kampuni ya M/S Mponela Construction Ltd kwa gharama ya shilingi Bil. 1.8.
MWISHO.
MENEJA wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA), Mkoa wa Simiyu Mhandisi Mariam
Majala, akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani) mara baada ya kukamilisha zoezi la utiaji saini wa miradi ya Maji mkoani Simiyu.

Post a Comment