Bil. 10 zatolewa kuongeza upatikanaji wa Maji Simiyu.

MENEJA wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA), Mkoa wa Simiyu Mhandisi Mariam Majala (aliyesimama) akishuhudia utiaji saini kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi ya Maji mkoani Simiyu.

 

Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.

 

SERIKALI kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA), Mkoa wa Simiyu imetoa kiasi cha shilingi Bil. 10 kwa ajili ya kutekeleza miradi minne ya Maji katika wilaya za Busega na Itilima.

 

Aidha katika mwaka wa fedha 2023/24, Wakala huyo ameidhinishiwa kiasi cha shilingi Bil. 32 kwa ajili ya kutekeleza miradi 32 ili kuongeza upatikanaji wa maji Mkoani humo.

 

Akizungumza jana mara baada ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa miradi ya maji, Meneja wa RUWASA, Mkoa wa Simiyu Mhandisi Mariam Majala alisema mara baada ya mikataba hiyo kusainiwa, wakandarasi watakabidhiwa maeneo ya kazi ndani ya siku saba.

 

Alifafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24 wameidhinishiwa kutekeleza miradi 32, lakini kwa sasa wamesaini kutekeleza miradi sita na ifikapo mwezi june 2024 miradi yote itakuwa imekamilika.

 
‘’Mikataba tuliyosaini leo, iwepo wakandarasi watatekeleza kwa muda mwafaka tutaongeza upatikanaji wa maji kwa kiasi kikubwa…tuko asilimia 70 kwa Mkoa mzima, na vijijini tuko asilimia 71 na tukikamilisha miradi hii tutaongeza asilimia 2 na ikikamilika yote 32 tutaongeza kwa asilimia 11 na kufikia asilimia 82 ifikapo June 2024’’ alisema.

Akimwakilisha Meneja wa RUWASA wilaya ya Itilima, Mhandisi Hassan Chambale alisema watahakikisha wanawasimamia wakandarasi ili watekeleze miradi ya maji kwa wakati.

 

Alisema wakandarasi hao wamekidhi vigezo vya kutekeleza miradi hiyo, hivyo wanatakiwa kutekeleza kwa wakati ili wananchi wapate maji safi na salama karibu na maeneo yao.

 

Awali Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika Mkoa huo.

 

Alisema wameshapatiwa zaidi ya shilingi Bil. 31 kwa ajili ya kutekeleza miradi 32 na kwamba wameanza kutekeleza miradi sita katika wilaya za Busega jumla ya vijiji 10 na Itilima vijiji vinne vitapatiwa huduma ya maji.

 
‘’Lengo letu la adhima ya Rais Samia kumtua mama ndoo kichwani tunaitimiza kwa asilimia 100, Miradi ya Maji ni miradi ya kipaumbele katika mkoa wangu, mmesaini leo kutekeleza kwa miezi 12, tungependa ikamilike kwa wakati’’ alisema Dk. Nawanda.

 
Katika wilaya ya Itilima, Mradi wa Chinamili na Sunzula utatekelezwa na Kampuni ya M/S AVCO BIZ LIMITED kwa gharama ya shilingi Bil. 2.1, Kinamweli na Madilina Kampuni ya M/S Pioneer Bulders Ltd kwa gharama ya shilingi Bil. 2.3.

 

Aidha katika wilaya ya Busega, Mradi wa Igalukilo na Kalemela utatekelezwa na kampuni ya M/S Ursino Ltd kwa gharama ya shilingi Bil. 3.7, wakati huo Mradi wa Kabita awamu ya pili utatekelezwa na Kampuni ya M/S Mponela Construction Ltd kwa gharama ya shilingi Bil. 1.8.

 

 MWISHO.

 

MENEJA wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA), Mkoa wa Simiyu Mhandisi Mariam Majala, akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani) mara baada ya kukamilisha zoezi la utiaji saini wa miradi ya Maji mkoani Simiyu.

 

 

Mkurugenzi wa Kampuni ya Orsino Limited Mnandi Mnandi akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) mara baada ya utiaji saini ya ujenzi wa miradi ya Maji katika wilaya za Busega na Itilima.

 

MENEJA wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA), Mkoa wa Simiyu Mhandisi Mariam Majala (katikati) akishuhudia utiaji saini kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi ya Maji mkoani Simiyu.

 

 

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم