Mapya yaibuka, Watoto Mapacha walifariki wakiongezewa Matiti.



Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

BABA Mzazi wa Pendo Kulwa Saku na Furaha Doto Saku, Mzee Yohana Saku, Mkazi wa Kijiji cha Bubale Kata ya Nkololo wilayani Bariadi Mkoani Simiyu amesema wakati vifo vya watoto wake vinatokea hakuwepo nyumbani badala yake alikuwa wilaya ya Maswa kwenye familia ndogo.

 

Saku ambaye ana familia mbili Maswa na Bariadi amesema hakuwa na taarifa yoyote juu ya watoto wake kupelekwa kwa mganga wa kienyeji na badala yake alipigiwa simu kuwa Pendo (Kulwa) anaumwa na kuwataka wampeleke hospitali.

 

Amesema alipata taarifa nyingine kutoka kwa mtoto wake mkubwa wa kiume kuwa mtoto wake mwingine Dotto naye anaumwa na kuwashauri naye wampeleke Hospitali.

 

“Baada ya kupata taarifa, niliwaambia wawampeleke hospitali lakini kumbe waliwapeleka kwa mganga wa kienyeji, baada ya muda mfupi nilipigiwa simu tena kuwa wamefariki’’ anasema na kuongeza.

 

‘’Nilipata taarifa pia kuwa na Furaha (Doto) amefariki wakati anapatiwa matibabu…nimeshangaa sana sababu nilikuwa sijui lolote na sihusiki katika haya’’.

 

Anaeleza kuwa baada ya kufika nyumbani kwake, hakuweza kupata muda wa kuzungumza na mke wake sababu alikuwa analia na kwamba baada ya muda alikamatwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi.

 

Amesema watoto wake walihitumu elimu ya sekondari na walikuwa wanajiandaa kwenda chuo cha ufundi Bunda kwa ajili ya kuendelea na masomo.

 

Ameongeza kuwa watoto hao mapacha ni kati ya watoto wake watano ambapo wasichana walikuwa wanne na mvulana alikuwa mmoja, hivyo wamebakiwa watoto watatu.

 

Watoto hao wawili  ambao ni Mapacha (17) wakazi wa kijiji cha Bubale kilichopo kata ya Nkololo wilayani Bariadi mkoani Simiyu waliopoteza maisha baada ya kupewa dawa na mganga wa tiba asili ili kuongeza matiti  waweze kuolewa, wamezikwa.

 

MWISHO.

 



 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post