Serikali: Mradi wa Shule bora umeanza kuleta tija.

 


Na Derick Milton, Simiyu.


Serikali imesema kuwa mradi wa SHULE BORA unaotekelezwa katika Mikoa tisa hapa nchini chini ya ufadhili wa serikali ya Uingereza kupitia mfuko wa UK Aid umeanza kuonyesha mafanikio makubwa katika maendeleo ya shule.


Mradi huo ambao unatekelezwa katika Shule za Msingi kwenye mikoa ya Simiyu, Tanga, Pwani, Dodoma, Singida, Mara, Kigoma, Katavi, na Rukwa unalenga kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua kiwango cha elimu.


Akiongoza timu ya viongozi na watalamu kutoka Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Elimu, wakiwemo wafadhili wa mradi huo kuangalia utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Simiyu.


Mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia Elimu ya watu wazima Wizara ya TAMISEMI Ernest Hinju amesema moja ya eneo ambalo mafanikio yamekuwa makubwa zaidi ni kuhimarishwa kwa mpango wa Ushirikiano wa Walimu na Wazazi Shuleni (UWAWA).


Amesema kuwa mradi wa Shule bora umesaidia sana kukomeshwa kwa utoro wa reja reja na uliokidhiri kwa wanafunzi, kwani wazazi wenyewe wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wote wanahudhuria shule siku zote.


 “ Tumetembelea baadhi ya shule kwenye mkoa wa Simiyu kuangalia utekelezaji wa mradi wa shule bora, kitu kikubwa ambacho tumekiona na kimekuwa bora zaidi ni kuhimalishwa kwa mpango wa Umoja wa Walimu na Wazazi (UWAWA), mpango huu umeleta maendeleo makubwa kwa shule zetu,” amesema Hinju…


“ Tumekuta Wazazi na walimu wamekuwa kitu kimoja, utoro umekomeshwa, wazazi wanachangia chakula shuleni kwa ajili ya watoto wao, maeneo mengine wamekarabati madarasa, tumefurahi kuona wananchi wanaona shule kama ya kwao,” ameeleza Hinju.


Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Simiyu, Afisa Elimu Mkoa Majuto Njanga amesema kuwa katika mkoa huo mradi wa shule bora umefanikisha kuanzishwa na mpango wa utoaji wa chakula shuleni hasa uji kwa shule zote za msingi mkoani humo.


“ Wazazi wameshirikishwa kupitia kamati za UWAWA kwa shule zote kwenye mkoa wetu, tumefanikiwa kutoa uji kwa kuanzia, lakini baadhi ya shule zinatoa na chakula cha mchana, mwitikio umekuwa mkubwa, hii imesaidia kupunguza mdondoko wa wanafunzi shuleni,” amesema Njanga.


Aidha Afisa Elimu huyo ameeleza kuwa mradi wa shule bora umesaidia kwa kiwango kikubwa kuwajengea uwezo walimu wa madarasa ya awali na darasa la kwanza kwa kuwapatia mbinu bora za ufundishaji.


“ Mradi pia umesaidia kuanzishwa kwa vituo vya utayari, ambapo mpaka sasa tuna vituo 24 mkoa mzima, vituo hivi vimekuwa muhimu sana kwa jamii, na vimepokea watoto wengi sana ambao walikuwa hawana uwezo wa kutembea umbali mrefu kufuata shule ilipo,” ameongeza Njanga.


Timu hiyo ikiwa katika shule ya Msingi Sapiwi ‘A’ iliyoko Wilayani Bariadi, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Henry Kitori amewaeleza kuwa kupitia UWAWA shule hiyo imefanikiwa kukarabati madarasa mawili ambayo yalikuwa yamechakaa.


Aidha Kitori amesema kuwa umoja huo umesaidia kuanzisha mradi wa ufugaji Mbuzi..” tilianza na mbuzi 10, lakini chini ya usimamizi wa UWAWA tuna mbuzi 31, ambao wanatumika katika maendeleo ya shule yetu”


Mwenyekiti wa UWAWA katika shule ya Msingi Nyakabindi Elia Shigalu akizungumza mbele ya timu hiyo, amesema kuwa jamii kwa sasa imetambua umuhimu wa kushiriki katika maendeleo ya shule.


“ Uko nyuma wengi tulidhani shule ni mali ya serikali, lakini kwa sasa wengi wameelimika kupitia hii UWAWA, tunashirikiana vyema na Kamati ya shule, shule yetu sasa hivi haina utoro tumekosema, watoto wetu wote wameanza kunywa uji, tumelima hekari nne kwa ajili ya chakula cha watoto wetu,” amesema Shigalu.



Mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia Elimu ya watu wazima Wizara ya TAMISEMI Ernest Hinju, akizungumza na walimu, wazazi katika shule ya Misngi Nyakabindi, iliyopo Wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post