Na Mwandishi wetu, Simiyu.
Kesi Namba 59
jinai, 2023 inayomkabili Askari wa Kituo cha Polisi Bariadi Mkoani Simiyu
H.4178 Abati Benedictor anayedaiwa kumpiga hadi kumsababishia majeraha mtoto
wake mwenye umri wa miaka 7 imeendelea tena jana katika Mahakama ya Wilaya ya
Bariadi mbele ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama hiyo Caroline Kiliwa.
Kesi hiyo
iliendelea kwa kusikilizwa Mashahidi upande wa Mashtaka, ambapo shahidi wa tatu
ambaye ni Daktari kutoka Hospitali ya Halmashuari ya Mji wa Bariadi (Somanda)
Nyangi Thomas alikuwa anatoa ushaidi wake.
Shahidi huyo ndiye
aliyehusika kumpokea na kumpatia matibabu mtoto huyo baada ya kufikishwa kwenye
hospitali hiyo kwa ajili ya kupatiwa huduma za kitabibu.
Akitoa ushahidi
wake Daktari huyo amesema kuwa mnano Januari 19, 2023 akiwa kazini Hospitali ya
Halmashuari ya Mji wa Bariadi, alimpokea mgonjwa ambaye ni mtoto akiwa
ameambatana na Askari pamoja na Mwalimu.
Amesema kuwa baada
ya kuwapokea, Askari huyo pamoja na Mwalimu walimweleza kuwa wamemleta mtoto
kwa ajili ya matibabu kutokana na majeraha aliyokuwa nayo sehemu mbalimbali za
mwili wake.
“ Nilimwangalia
mtoto na nikamhoji kuhusu anachoumwa, alinieleza kuwa ana maumivu mgongoni,
nilimuuliza mtoto maiumivu hayo yanatokana na Nini? Alinieleza kuwa alipigwa na
mzazi wake wakati akimfundisha masomo,” amesema Daktari.
Shahidi huyo aliendelea
kuelezea mahakama kuwa baada ya maelezo ya mtoto, aliamua kumfanyia uchunguzi
wa awali na kubaini ana maumivu sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo
mgongoni.
Aidha Daktari huyo
alieleza kuwa alibaini macho ya mtoto huyo yalikuwa na upungufu wa damu, mgongo
ulikuwa umevimba, vidonda alivyokuwa navyo mgongoni vilikuwa na urefu wa
sentimeta saba (7) na Upana Sentimeta tano (5).
“ Majeraha mengine
yalikuwa rangi nyekundu na megine nyeusi, baadhi niliyashika yalikuwa na usaha,
Sikio la kushoto kwa nyuma lilikuwa na kidonda kikubwa ambacho kilikuwa kinatoa
damu,”
Aidha alisema kuwa
miguu ya mtoto huyo ilikuwa imevimba, baada ya kumchunguza alimfanyia vipimo
kisha akampatia dawa za maimivu za sindano, lakini pia alipiga simu kuomba
afisa wa ustawi wa jamii awepo.
“ Baada ya majibu
ya vipimo kutoka, mtoto alibainika kuwa ana upungufu wa damu, lakini alikuwa na
maambukizi katika mfumo wake wa damu, nikaamua alazwe ili apate matibabu zaidi,
kisha nikajaza fomu ya PF3,”
Shahidi huyo
alipoulizwa na Mwendesha mashtaka wa serikali Rehema Sakafu kuhusu fomu hiyo
kama anaikumbuka endapo ataonyeshwa, alisema anaikumbuka kwa kutambua mwandiko
wake, mhuri wa mganga mkuu, na namba yake ya usajili aliyoandika.
Mwendesha Mashtaka
alipomwesha fomu hiyo Shahidi huyo alikiri kuwa ndiyo yenyewe aliyojaza wakati
anampatia matibabu mtoto huyo, ambapo aliomba Mahakama kuipokea fomu hiyo kama
kielelezo kwenye kesi hiyo.
Mwendesha Mashtaka
alimtaka shahidi kusoma maelezo ya fomu hiyo ambayo alijaza mbele ya mahakama.
Shahidi huyo
alianza kusoma maelezo hayo, ambapo aliandika kuwa Askari na Mwalimu ambao
walimleta mtoto Hospitali walimweleza kuwa majeraha aliyokuwa nayo mtoto
yalisababishwa na kupigwa na baba yake.
Aliendelea kusoma
fomu hiyo, namna alivyomtibu mtoto, ambapo katika maoni yake ya mwisho
(Conclusion) kwenye fomu hiyo alieleza Majeraha aliyokuwa nayo mtoto yalitokana
na kupigwa na kusababisha vidonda ambavyo vinaweza kuhitaji apandikizwe ngozi
lakini pia mtoto atahitaji matibabu ya kisaikologia.
Baada ya kusikiliza
kwa Shahidi huyo, Hakimu alihailisha kesi hiyo hadi Novemba 02, 2023 kesi hiyo
itakapoendelea kusikilizwa tena.
Askari huyo
akabiliwa na shtaka moja ambalo ni kumchapa mtoto wake kwa fimbo na kumjeruhi
maeneo mbalimbali ya mwili wake kinyume na kifungu Cha 169 A kifungu kidogo Cha
1 na Cha 2 Cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 marejeo ya mwaka
2022.

Post a Comment