Shahidi Kesi ya Askari kumjeruhi mtoto: Majeraha aliyokuwa nayo mtoto yalitokana na kupigwa

 



Na Mwandishi wetu, Simiyu.


Kesi Namba 59 jinai, 2023 inayomkabili Askari wa Kituo cha Polisi Bariadi Mkoani Simiyu H.4178 Abati Benedictor anayedaiwa kumpiga hadi kumsababishia majeraha mtoto wake mwenye umri wa miaka 7 imeendelea tena jana katika Mahakama ya Wilaya ya Bariadi mbele ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama hiyo Caroline Kiliwa.


Kesi hiyo iliendelea kwa kusikilizwa Mashahidi upande wa Mashtaka, ambapo shahidi wa tatu ambaye ni Daktari kutoka Hospitali ya Halmashuari ya Mji wa Bariadi (Somanda) Nyangi Thomas alikuwa anatoa ushaidi wake.


Shahidi huyo ndiye aliyehusika kumpokea na kumpatia matibabu mtoto huyo baada ya kufikishwa kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kupatiwa huduma za kitabibu.


Akitoa ushahidi wake Daktari huyo amesema kuwa mnano Januari 19, 2023 akiwa kazini Hospitali ya Halmashuari ya Mji wa Bariadi, alimpokea mgonjwa ambaye ni mtoto akiwa ameambatana na Askari pamoja na Mwalimu.


Amesema kuwa baada ya kuwapokea, Askari huyo pamoja na Mwalimu walimweleza kuwa wamemleta mtoto kwa ajili ya matibabu kutokana na majeraha aliyokuwa nayo sehemu mbalimbali za mwili wake.


“ Nilimwangalia mtoto na nikamhoji kuhusu anachoumwa, alinieleza kuwa ana maumivu mgongoni, nilimuuliza mtoto maiumivu hayo yanatokana na Nini? Alinieleza kuwa alipigwa na mzazi wake wakati akimfundisha masomo,” amesema Daktari.


Shahidi huyo aliendelea kuelezea mahakama kuwa baada ya maelezo ya mtoto, aliamua kumfanyia uchunguzi wa awali na kubaini ana maumivu sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo mgongoni.


Aidha Daktari huyo alieleza kuwa alibaini macho ya mtoto huyo yalikuwa na upungufu wa damu, mgongo ulikuwa umevimba, vidonda alivyokuwa navyo mgongoni vilikuwa na urefu wa sentimeta saba (7) na Upana Sentimeta tano (5).


“ Majeraha mengine yalikuwa rangi nyekundu na megine nyeusi, baadhi niliyashika yalikuwa na usaha, Sikio la kushoto kwa nyuma lilikuwa na kidonda kikubwa ambacho kilikuwa kinatoa damu,”


Aidha alisema kuwa miguu ya mtoto huyo ilikuwa imevimba, baada ya kumchunguza alimfanyia vipimo kisha akampatia dawa za maimivu za sindano, lakini pia alipiga simu kuomba afisa wa ustawi wa jamii awepo.


“ Baada ya majibu ya vipimo kutoka, mtoto alibainika kuwa ana upungufu wa damu, lakini alikuwa na maambukizi katika mfumo wake wa damu, nikaamua alazwe ili apate matibabu zaidi, kisha nikajaza fomu ya PF3,”


Shahidi huyo alipoulizwa na Mwendesha mashtaka wa serikali Rehema Sakafu kuhusu fomu hiyo kama anaikumbuka endapo ataonyeshwa, alisema anaikumbuka kwa kutambua mwandiko wake, mhuri wa mganga mkuu, na namba yake ya usajili aliyoandika.


Mwendesha Mashtaka alipomwesha fomu hiyo Shahidi huyo alikiri kuwa ndiyo yenyewe aliyojaza wakati anampatia matibabu mtoto huyo, ambapo aliomba Mahakama kuipokea fomu hiyo kama kielelezo kwenye kesi hiyo.


Mwendesha Mashtaka alimtaka shahidi kusoma maelezo ya fomu hiyo ambayo alijaza mbele ya mahakama.


Shahidi huyo alianza kusoma maelezo hayo, ambapo aliandika kuwa Askari na Mwalimu ambao walimleta mtoto Hospitali walimweleza kuwa majeraha aliyokuwa nayo mtoto yalisababishwa na kupigwa na baba yake.


Aliendelea kusoma fomu hiyo, namna alivyomtibu mtoto, ambapo katika maoni yake ya mwisho (Conclusion) kwenye fomu hiyo alieleza Majeraha aliyokuwa nayo mtoto yalitokana na kupigwa na kusababisha vidonda ambavyo vinaweza kuhitaji apandikizwe ngozi lakini pia mtoto atahitaji matibabu ya kisaikologia.


Baada ya kusikiliza kwa Shahidi huyo, Hakimu alihailisha kesi hiyo hadi Novemba 02, 2023 kesi hiyo itakapoendelea kusikilizwa tena.


Askari huyo akabiliwa na shtaka moja ambalo ni kumchapa mtoto wake kwa fimbo na kumjeruhi maeneo mbalimbali ya mwili wake kinyume na kifungu Cha 169 A kifungu kidogo Cha 1 na Cha 2 Cha Sheria ya kanuni ya adhabu  sura 16 marejeo ya mwaka 2022.


 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم