​TARI Nyakabindi yawanoa wakulima kuogeza thamani mazao ya mizizi.

Baadhi ya wakulima kutoka Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, wakiendelea na kuandaa vyakula vitokanavyo na mazao ya mizizi, baada ya kupata mafunzo kutoka kwa watalaamu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ya jinsi ya kuongeza thamani kwenye mazao hayo.

 

Na Derick Milton, Simiyu.

 

Katika kuhakikisha wakulima wananufaika na mazao yao Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo chake cha usambazaji wa Teknologia bora za kilimo(Nyakabindi Hub) kilichopo katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu imetoa mafunzo kwa wakulima jinsi ya kuongeza thamani kwenye mazao ya mizizi.

 

Mafunzo hayo ambayo yalikuwa ya siku moja, yameongozwa na mtafiti mwandamizi kutoka TARI Ukiriguru Mkoani Mwanza, Dkt. Caresma Chuwa ambapo yamewashirikisha wakulima zaidi ya 200 wengi kutoka katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.

 

Dkt. Chuwa amesema kuwa lengo la mafunzo hayo, ni kuona wakulima wananufaika na kilimo chao kwa kupata elimu ya jinsi ya kuongeza thamani na siyo kuuza kama ambavyo wamezoa ambapo wengi wanauza kwa bei ndogo

 

“ Tunajua kabisa wakulima hasa wa mazao ya mizizi wakivuna wanauza kwa bei ndogo bila ya kuongeza thamani, wengi hawana hii elimu, kama wadau wakubwa wa kilimo nchini, tumeona kuja na elimu hii kuwafundisha jinsi ya kuongeza thamani viazi, pamoja na mohogo, ili wajiongezee kipato,” amesema Dkt. Chuwa.

 

Amesema kuwa uwekezaji kwenye kilimo unanzia kwenye mbegu, kanuni bora za kilimo, kuvuna kwa ufasaha kisha kuongeza thamani ya mazao yenyewe, jambo ambalo ameeleza wakulima wengi hawafanyi.

 

“ Kwa elimu hii wengi wameelewa, vyakula na mahitaji yote ya kuongeza thamani wana uwezo wa kuyapata, hawa ambao tumewapa elimu hii watakuwa walimu wazuri wa wengine na tunaamini kuwa sasa wakulima watanufaika na kilimo chao,” amesema Dkt. Chuwa.

 

Nao wakulima waliopata mafunzo hayo wameishukuru TARI kwa elimu ambayo wameipata, ambapo wameeleza kwa mara kwanza waliowengi hawakuwa na elimu ya jinsi ya kuongeza thamani mazao ya mizizi kama mihogo na viazi.

 

“ Tunashukuru sana watu wa TARI kwa Elimu hii, wengi nikiwemo mimi hatukuwa na elimu ya jinsi ya kuongeza thamani mazao yetu hasa viazi, kwa mafunzo haya kama mkulima naweza kuongeza thamani mazao yangu,” amesema Juliana Mayenga.

 

Naye Agness Joseph Mkulima wa Nyakabindi Mbali na kushukuru TARI kwa mafunzo hayo amewaomba kuendelea kutoa mafunzo kwa wakulima wengine ambao hawakupata mafunzo hayo.

 

Mafunzo hayo ambayo yamefanyika jana katika kituo hicho yalilenga zaidi mazao ya mhogo, ndizi, viazi vitamu pamoja na viazi lishe, huku wakulima wakifundishwa pia jinsi ya kupika makande kwa kuchanganya maharage na mbogamboga

 

Mtafiti mwandamizi kutoka TARI Ukiriguru Mkoani Mwanza, Dkt. Caresma Chuwa akiendelea kutoa mafunzo kwa wakulima mbalimbali wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu kwenye kituo cha usambazaji wa Teknologia za kilimo Nyakabindi jinsi ya kuongeza thamani kwenye mazao yatokanayo na mizizi.





Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post