CCM yawapongeza Alliance Ginnery Upandaji Miti.

 MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bariadi Juliana Mahongo (kulia) akimpongeza Meneja wa Kiwanda cha Kuchambua pamba cha Alliance Ginnery Boaz Ogolla kwa kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika utunzaji wa mazingira na upandaji miti.

 


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bariadi Juliana Mahongo (kulia) akizungumzia juhudi za Upandaji miti na Utunzaji wa Mazingira zinazofanywa na Kiwanda cha Kuchambua Pamba cha Alliance Ginnery, kushoto ni Meneja wa kampuni hiyo Boaz Ogolla




 
KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bariadi Masanja Salu akishiriki zoezi la Upandaji miti katika shule ya msingi Dk. Otto iliyoko Kasoli, wakati wa sherehe za Maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa CCM yaliyofanyika kata ya Kasoli.
 
 

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bariadi Juliana Mahongo (wa pili nyuma) akipanda mti katika shule ya msingi Dk. Otto iliyoko Kasoli kwenye maadhimisho ya miaka 46 ya CCM yaliyofanyika kata ya Kasoli.


 

Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu kimeipongeza Kampuni ya Ununuzi wa Pamba ya Alliance Ginnery iliyoko Kijiji cha Kasoli wilayani humo kwa jitihada zake za kupanda miti na kutunza Mazingira.

 

Mbali na Ununuzi wa Pamba, Kampuni hiyo imekuwa ikiandaa vitalu na kuotesha miti ya aina mbalimbali kwa lengo la kuwagawia bure Wananchi, Taasisi za Umma na Madhehebu ya dini ili kupanda katika maeneo yao kwa lengo la kulinda na kutunza uoto wa asili.

 

Hayo yamebainishwa leo na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bariadi Juliana Mahongo mara baada ya kukagua vitalu vya miti kiwandani humo, kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 46 ya Kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika Kata ya Kasoli.

 

Amesema kampuni hiyo inaunga mkono juhudi za Rais Samia kuhusu uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali zikiwemo Taasisi za Umma, Madhehebu ya dini pamoja na kugawa bure kwa wananchi.

 

‘’Niombe uendelee na moyo huohuo wa kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu…wanunuzi wa Pamba wangekuwa na moyo huu, mkoa wetu ungekuwa na miti mingi sana, kwa maana amesambaza mkoa mzima na mkoa jirani wa Mwanza’’ amesema Juliana.

 

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo ameipongza kampuni ya Alliance Ginnery kwa namna inavyoshirikiana na serikali kuchangia shughuli za maendeleo kwa kujenga miundombinu katika sekta za elimu, afya, maji na barabara.

 

Kwa upande wake Meneja wa Kiwanda cha Alliance Boaz Ogolla amesema wameamua kumuunga mkono Rais Samia kwa kuanzisha kitalu cha miti ili wilaya ya Bariadi iwe na miti ambayo inagawiwa bure.

 

‘’Kuna vitalu vitatu, kimoja kina miche laki tatu, kingine miche laki mbili na hamsini…lengo letu ni kuibadilisha Simiyu kuwa ya kijani na kumuunga mkono Rais Samia kwa kupanda miti laki sita, tuna miche ya mbao, matunda, kivuli na miti ya kulisha mifugo na kurutubisha ardhi’’ alisema Ogolla.

 

Amefafanua kuwa wamesambaza katika taasisi za shule, misikiti na makanisa, pia wameanzisha vitalu katika vijiji vya Ngala, Ngulyati na Mbiti na wilaya ya Busega na kwamba wananchi wa vijiji vinavyozunguka kiwanda hicho wanapatiwa miti bure.

 

MWISHO.

 

 

 Vijana wakipanda miti.

 

 

 Kitalu cha miti aina ya Mwarobaini kilichopo katika kiwanda cha Kuchambua Pamba cha Alliance Ginnery.


 

 

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post