Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
WATOTO Wawili ambao ni Mapacha (17) wakazi wa kijiji cha Bubale kilichopo kata ya Nkololo wilayani Bariadi mkoani Simiyu waliopoteza maisha baada ya kupewa dawa na mganga wa tiba asili ili kuongeza matiti waweze kuolewa, wamezikwa.
Watoto hao waliofahamika kwa majina ya Pendo (Kulwa) Saku na Furaha (Doto) Saku wamezikwa na mamia ya wananchi waliojitokeza kushiriki mazishi hayo.
Akizungumza wakati akitoa salamu za pole kwenye msiba huo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Kata ya Nkololo Agnes Chalimaga amewataka wananchi hao kujifunza juu ya matukio yanayotekea katika jamii.
‘’Tujifunze kwa waliobaki, siyo kila jambo kwenda kwa mganga wa kienyeji…hakikisheni mnaachana na taama za kidunia, tuendelee kufarijiana wakati taratibu za kiserikali zinaendelea’’ amesema.
Diwani wa Kata ya Nkololo Emmanuel Nyawela amesema vijana hao walikuwa wamefikia umri wa kuwatumikia watanzania kwa kupata madaraka mbalimbali, lakini maisha yao yamefikia ukomo.
Ameitaka jamii kuendelea kufarijiana wakati huo wakiachana na mila potofu ambazo zinasababisha mauji na Imani za kishirikina ikiwemo kuwaamini zaidi waganga wa kienyeji.
Diwani wa Viti Maalumu, Kata ya Nkololo Helena Itabaja amesema matukio kama hayo walikuwa wanayaona kwenye televisheni yakitokea kwingineko, lakini leo yametokea kijijini hao.
Amewataka wananchi kuendelea kumwamini Mungu na kuacha kujihusisha na Imani za kishirikina zinazosababisha mauaji katika jamii kwa sababu hawana taaluma yoyote kuhusu madawa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bubale Masebu Lubugwa ameiwataka waganga wa kienyeji kuacha kutibu magonjwa ambayo hawana uwezo nayo na baadala yake watumie madaktari kwenye vituo vya afya na zahanati.
‘’Tunaiomba serikali ichukue mkondo wake, waganga waache kutibu magonjwa ambayo hawana uwezo…jamii tujenge ulewa wa pamoja ili tunusuru jamii yetu’’ amesema.
MWISHO.
Post a Comment